Dear Ankal,
Kwanza nikupe Big UP!!! sana kwa kuendesha blog yetu kwa weledi wa hali ya juu. Yaani ma-news kila dakika na up-to-date kama CNN mwanangu. Hakika unatisha na hakuna wa kukufikia kaka. Halafu unanikoshaga kwa kutoweka mambo ya udaku, umbea na majungu...
La pili ni kukupongeza kutoa nafasi kwa wadau kutoa madukuduku yao bila chenga. Yaani yule jamaa wa juzi wa Norway anayepima zali la kuja kuomba visa ya Marekani baada ya kuopoa Green Card ni funika bovu. Ndio maana na mimi leo najikunja kuomba ushauri toka kwa wadau wako lukuki duniani kote, japo shida yangu ni tofuti na ya mdau wa visa wa Norway ambaye nami namshauri asinoe stepu na kuhamia Marekani. Mie niko huku mwaka wa 28 leo, na Green Card yangu, lakini acha! Kufa sifi ila cha moto nakiona. Nna kila kitu ila sina mwenza wa kufurahi nae...
Mie Ankal naishi East Coast huku (kwa sasa jina la mji kapuni, wambea naogopa wasinichore). Tatizo langu natafuta mwenza kutoka nyumbani Tanzania, tatizo sijafika huko miaka yote hiyo na pa kuanzia sijui (wazazi wangu wote wametangulia mbele ya haki). Ndugu zangu wengi nimepoteza mawasiliano nao (waliniliza pesa nilizowatumiaga za kujengea, wamezila na wakakata mawasiliano) hivyo sina uhakika kama wote wapo. Nilikuwa naishi Kariakoo, Dar, mtaa wa Narung'ombe, ila katika taswira moja ulioonesha siku za hivi karibuni nimeona nyumbani petu pana bonge la kikwangua anga. Najua tu kuwa jamaa zangu ndio wameshauza nyumba yetu na kulala mbele.
Samahani kama nawakwaza kwa hadisi ndefu ila shida yangu ndiyo hiyo. Nataka kurejea nyumbani mara moja kuja kusaka wa kuishi naye. Mie sasa nagota miaka 51 ila bado niko fiti kila idara, ikiwa ni pamoja na pesa ya kubadili mboga kila siku hainipigi chenga. Maana boxi ninalokula huku si haba. Niliwahi kuishi na mfilipino na baadaye Mvenezuela lakini tukazinguana sasa niko alone. Mfilipino nilizaa naye watoto wa kiume wawili, kakimbia nao kwenda wapi sijui. Huyu mwingine hatukubahatika.
Sasa basi, shida yangu ni wapi pa kuanzia pindi nikija huko??? Halafu huyo mchumba, ambaye sina tatizo la dini wala elimu yake (awe na angalau ya fom foo tu, tosha!), nitampataje wakati nikija nitakuwa mgeni na muda wangu ni wiki tatu tu???
Naomba mchango wa mawazo toka kwa wadau nifanyeje nipate mwenza wa Kitanzania toka nyumbani Tanzania?? Nikija nianzie wapi?? Kuna agency za kutatua matatizo kama hayo huko???
Mdau
East Coast, USA