Mh.Waziri Mkuu Pinda.
*Akemea matumizi mabaya, kupendelea na kujipa tenda
*Ahimiza usimamizi wa fedha wa umma
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amecharuka na kuwakemea watendaji kwenye Serikali za Mitaa ambao wanatumia nafasi zao kulazimisha kufanya biashara na Halmashauri wanazoziongoza.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Mei 9, 2013) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 29 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika hoteli ya Sundown Carnival, nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Waziri Mkuu alisema haipendezi kusikia baadhi ya wakuu na watendaji katika Halmashauri wakituhumiwa kuwa sehemu ya mitandao ya wizi katika Halmashauri au wana maslahi katika kampuni zilizohusika kutoa huduma na bidhaa duni kwa Halmashauri.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema kuna malalamiko amepokea kwamba Meya wa Halmashauri moja amefungua kampuni sita na zote anataka zipewe tenda kwenye Halmashauri anayoiongoza.
“Kuna Halmashauri zenye taarifa za wizi, upotevu na ubadhirifu ambao kwao umekuwa ni maisha ya kawaida. ALAT mnayo nafasi kubwa kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha za Halmashauri kwa vile Jumuiya yenu inawaunganisha watendaji wakuu na viongozi wakuu wa Halmashauri zote chukueni hatua. Waaibisheni na kuwaumbua wale wanaobanika kutumia vibaya fedha hizi za umma.”
“Lakini, ili muweze kufanya hayo lazima ninyi wenyewe msiwe sehemu ya uovu huu. Inafadhaisha sana kusikia minong’ono kuwa baadhi ya madiwani wanatuhumiwa kuwa sehemu ya mitandao ya wizi katika Halmashauri .... huo ni ukosefu wa wajibu na ni kuvunja mkataba wenu na umma.
Akuzungumzia kuhusu utunzaji wa mahesabu, Waziri Mkuu alisema upo udhaifu katika eneo hilo kwani upo ushahidi unaoonesha kwamba taarifa za vitabuni hazifanani na kazi iliyofanywa (value for money) akimaanisha kwamba kazi inayofanyika hailingani na thamani halisi ya fedha iliyotumika.
“Tatizo hili ni kubwa na lina sura mbili kuu. Moja ni kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watumishi na madiwani katika usimamizi wa fedha za Serikali za Mitaa. Baadhi ya madiwani wamediriki kushirikiana na watumishi wasio waaminifu katika kuhujumu fedha za umma. Pili, ni Watumishi wa Serikali za mitaa kushindwa kutekeleza wajibu wao hivyo kulipwa mishahara ambayo hawaitumikii ipasavyo,” alisema.
“Hili nalo nataka lijadiliwe kwa kina na mkitoka hapa kila Kiongozi na Mtendaji ajue ana jukumu gani la kufanya. Aidha, hili ndilo eneo ambalo nataka hatua zichukuliwe ili kunusuru Fedha za Halmashauri,” alisisitiza.
Alisema kwa kutambua ukweli huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameendelea na ukaguzi wa thamani ya fedha zaidi ya ukaguzi wa kawaida.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alipokea hundi ya mfano ya sh. milioni 10 iliyotolewa na Benki ya NMB ili ziweze kusaidia kununua dawa na vifaa tiba kwa ajili ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu mkoani Arusha kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea Mei 5, mwaka huu kwenye Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti.
Akizungumzia msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Serikali wa benki hiyo, Bibi Domina Feruzi alisema, kama taasisi wameguswa na maafa yaliyowakumba wakazi hao wa Arusha na wameamua kuchangia kiasi hicho cha fedha ili kiwasaidie kwa dawa na vifaa vya tiba vinayohitajika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MEI 9, 2013.