Na. Eliphace Marwa - MAELEZO
Serikali imesema kuwa itaendelea kutumia njia mbalimbali kuwahamasisha wananchi kuzingatia matumizi ya lishe bora kwa kuweka msisitizo katika kilimo cha matunda, mbogamboga, ufugaji wa samaki na matumizi ya vyakula vilivyowekewa virutubisho muhimu .
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri mkuu Peniel Lyimo akiongea na
waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu mkuu Kiongozi ,leo jijini Dar es salaam amesema kuwa hali ya lishe nchini hairidhishi na tatizo la utapiamlo limeeendelea kuiathiri jamii ya watanzania.
Amesema takwimu za mwaka 2010 zinaonesha kuwa asilimia 42 ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano wamedumaa, asilimia 16 wana uzito pungufu na asilimia tano wamekonda.
Aidha amesema asilimia 59 ya watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi 59 wana upungufu wa damu, asilimia 33 ya watoto chini ya miaka sita wana upungufu wa vitamin A”, alisema Lyimo.
Pia ameongeza kuwa asilimia ya wanawake walio katika umri wa kuzaa yaani miaka 15 hadi 49 wanapata changamoto mbalimbali za kiafya zinazosababishwa na lishe duni za upungufu wa damu, matatizo ya ukosefu wa madini joto mwilini, upungufu wa uzito na baadhi ya mama wajawazito kuwa na tatizo la ukosefu wa vitamini A.
Pia ameeleza kuwa tatizo la utapiamlo unaotokana na ulaji unaozidi mahitaji kilishe linaendelea kuongezeka na unaathiri zaidi kwa wakazi wa mijini na tatizo hili hupelekea magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama moyo, kisukari na kansa.
Kwa upande wake Msaidizi wa Rais masuala ya lishe Dkt Wilbald Lorri amesema kuwa ufumbuzi wa tatizo la lishe bora kwa jamii liko mikononi kwa wanajamii wenyewe kujenga tabia ya kula matunda na mbogamboga vitu ambavyo hupatikana kwa wingi na urahisi katika maeneo yao.
Amefafanua kuwa serikali imeweka msukumo katika kukamilisha mkakati wa taifa wa lishe pamoja na mpango wake wa utekelezaji, kuanzisha kamati ya kitaifa ya ushauri wa lishe nchini, kuanzisha dawati la lishe katika halmashauri zote nchini pamoja na kuanzisha kasma ya lishe katika bajeti ya halmashauri,kuingiza na kuimarisha masuala ya lishe katika kilimo na uongezaji wa virutubisho katika mafuta ya kula, unga wa ngano na unga wa mahindi.
Aidha wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo yatayofanyika kuanzia mei 15 na kufikia kilele chake mei 16 katika viwanja vya Mnazi mmoja yakiongozwa na kauli mbiu isemayo " Lishe bora ni Msingi wa Maendeleo , Timiza Wajibu wako"
ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya atazindua kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya Lishe bora.