Na: Eliphace Marwa – Maelezo
CHAMA cha wauguzi Tanzania kinatarajia kufanya maadhimisho ya siku ya waaguzi duniani mei 12 ambapo kitaifa yatafanyika mkoani Rukwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Rais wa chama hicho bwana Paulo Magesa alisema maadhimisho hayo yatafanyika tarehe 12 mei ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Kuziba pengo kufikia Malengo ya Milenia namba 6,5,4”.
Bwana Magesa alisema malengo hayo ya millennia yanalenga kuzuia vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua , kuzuia vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Pamoja na changamoto nyingi tunazokutana nazo wauguzi bado tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuhakikisha huduma bora zinawafikia walengwa na hii imeleta mafanikio makubwa kwani vifo vya mama wajawazito pamoja na watoto vimepungua sana”, alisema bwana Magesa.
Wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa ajili ya kuzuia na kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto nchini chini ya mpango huu umelenga kuhamasisha akina mama kutumia njia salama za uzazi wa mpango na kuhakikisha wanajifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za mama na mtoto.
Aidha, kwenye maadhimisho hayo kutakuwa na maonesho kuanzia tarehe 10 hadi 12 mei yakionesha shughuli mbalimbali za kitaaluma wanazozifanya wauguzi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kiafya kama huduma ya mama na mtoto, huduma za kupima VVU na ushauri nasaha na huduma nyingine nyingi.
Chama cha wauguzi Tanzania (TANNA) ni chama kinachowawakilisha wauguzi na wakunga wote Tanzania bara na Katika maadhimisho hayo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr. Hussein Mwinyi.