KAMATI ya kusimamia Tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2012 zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imepokea mapendekezo ya majina ya wanamichezo kutoka vyama mbalimbali kwa ajili ya kuwania tuzo hizo kwa kila mchezo.
Majina ya wanamichezo hao yamependekezwa na vyama husika, isipokuwa mpira wa miguu kwa wanaume pamoja na mpira wa kikapu, ambapo majina yameteuliwa na kamati kwa kushirikiana na baadhi ya wahariri wa habari za michezo na wadau wa michezo husika, ingawa awali vyama hivyo viliombwa kuwasilisha majina lakini havikutekeleza ombi hilo hivyo kamati ikaamua kutafuta utaratibu mwingine wa kupata majina.
Pia vyama viwili vya michezo ya paralimpiki na baiskeli bado majina hayajaifikia kamati yetu kutokana na sababu mbalimbali na tayari wameahidi watawasilisha majina hayo kabla ya Mei 12 mwaka huu. Chama cha Mpira wa Wavu pia kimeshindwa kuwasilisha majina.
Hatua ya mwisho ambayo itafanyika baada ya kupokea mapendekezo hayo kwenye kila mchezo, Kamati ya Tuzo za Taswa itafanya uchambuzi kupitisha majina hayo kulingana na sifa ambazo vyama husika vimeleta kwa kila mwanamichezo na kuona kama wanastahili kupewa tuzo kulingana na vigezo vya kamati na TASWA.