Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiongozana na balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, ofisini kwake Migombani. Picha na Salmin Said, OMKR |
Na Hassan Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameihakikishia Canada kuwa Zanzibar ina maeneo mazuri ya kuwekeza na kuwaomba wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza katika Nyanja tofauti zikiwemo ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii, kumbi za mikutano na uvuvi wa bahari kuu.
Amesema Zanzibar ina mahitaji makubwa ya uwekezaji katika maeneo hayo, na kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa taifa na kunyanyua kipato cha wananchi.
Akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania balozi Alexandre Leveque ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema serikali imelenga kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza miradi mbali mbali ya kiuchumi.
Aidha Maalim Seif ameiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kuleta wataalamu wa Afya na walimu wa sayansi, ili kupunguza tatizo la wataalamu hao nchini.
Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta hizo, lakini bado zina upungufu wa wataalamu wakiwemo madaktari wenye sifa, pamoja walimu wa masomo ya sayansi.
Amesifu mchango wa nchi hiyo hasa katika sekta za afya na elimu na kutaka isichoke kutoa misaada yake katika kusaidia kunyanyua uchumi wa Zanzibar.
Kwa upande wake balozi Alexandre amesema Canada imekuwa ikihamasisha wawekezaji binafsi, na kuahidi kuwahamisha kuja kuwekeza Zanzibar.
Kuhusu upatikanaji wa wataalamu wa Afya na walimu wa Sayansi, balozi huyo amesema atawasiliana na mamlaka zinazohusika, ili kupata wataalamu wakiwemo wa kujitolea, watakaoweza kuja kufanya kazi katika maeneo hayo.
Amesema Canada inajivunia uhusiano wa muda mrefu uliopo kati yake ya Zanzibar, na kwamba uhusiano huo utaendelezwa kwa maslahi ya pande hizo mbili.