Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania-TRL unapenda, kupitia taarifa hii, kukanusha taarifa zilizochapishwa katika majarida ya Kulikoni la tarehe Aprili 26 – Mei 2 na Fahamu la tarehe 26, April, 2013 kuwa mchakato wa ununuzi wa Vichwa 13 vya treni ulikuwa na utata.
Ukweli ni kwamba Zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni 13 ilitangazwa kwenye magazeti mbalimbali tarehe 9 na 10 Novemba, 2012. Kabla ya siku ya kufungua zabuni hii ambayo ilikuwa ni tarehe 1 Februari, 2013, TRL ilipokea barua kutoka PPRA iliyopokelewa tarehe 31 Januari, 2013 ambayo iliambatanisha barua ya malalamiko kutoka kwa Kampuni moja ikilalamika kuwa TRL ilikuwa imekiuka Sheria ya Manunuzi kwa kuweka vipengele kwenye zabuni ambavyo viliiengua kampuni hiyo isiweze kushiriki kwenye zabuni.
Baada ya kupokea barua ya PPRA, TRL ilitathmini hoja ya mlalamikaji kwa kupitia Sheria aliyoitaja pamoja na nyaraka mbalimbali zilizokuwepo. Baada ya tathmini hii TRL ilbaini mambo yafuatayo:
a) Mlalamikaji hakuwa miongoni mwa makampuni yaliyokuwa yamenunua nyaraka za zabuni.
b) Mlalamikaji alijikita kwenye suala la aina tano tofauti za injini zilizopendekezwa na TRL kutumika kwenye vichwa hivyo vya treni bila kuzingatia kuwa zabuni hii haikuwa ya ununuzi wa injini bali vichwa vya treni. Katika zabuni hii TRL haikuweka masharti yoyote yanayozuia kampuni yoyote duniani kutengeneza vichwa hivyo vya treni.
c) Katika barua yake ya malalamiko alieleza kuwa kabla ya kuandika barua kwenda PPRA alikuwa ametuma barua nyingine kwenda TRL akiomba aina ya injini inayotengezwa na kampuni anayoiwakilisha itajwe kama moja ya injini ambazo zingeweza kufungwa kwenye vichwa vya treni ambavyo vingenunuliwa na TRL. Hata hivyo barua aliyoitaja haikuwa imepokelewa na TRL.
d) TRL ilijiridhisha kuwa haikuwa imekiuka Sheria ya Manunuzi.
Baada ya tathmini hii TRL ilipeleka maelezo yake PPRA kwa barua ya tarehe 4 Februari, 2013.
Ifahamike kwamba taratibu za Rufaa katika Sheria ya Manunuzi ziko wazi. Kama mlalamikaji huyu angekuwa na nia ya kweli kutaka kupata haki yake angefuata utaratibu wa Rufaa ambao umeainishwa katika Sheria hiyo hiyo ya Manunuzi badala ya kutumia vyombo vya habari.
Uamuzi wa mlalamikaji kutofuata taratibu za kisheria na kuamua kupeleka tuhuma kwenye vyombo vya habari unaonekana ni uamuzi wa kupakana matope ambao hauna tija kwa mlalamikaji, TRL na jamii kwa ujumla.
Aidha tunatoa rai kwa vyombo vya habari kutokubali kuandika habari kabla ya kuzifanyia utafiti kwani kwa kufanya hivyo jamii ya Watanzania inapotoshwa kwa kiasi kikubwa sana.
-Mwisho-
Imetolewa na Afisi ya Uhusiano
kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL,
Mhandisi Kipallo Aman Kisamfu
Dar es Salaam
Aprili 30, 2013