Jengo la ghorofa nane lililokuwa na viwanda vya nguo na maduka limeporomoka leo mchana nje ya jiji la Dhaka, Bangladesh, na kuua watu takriban 100 na kujeruhi wengine zaidi ya 1000, maafisa wamesema.
Vikosi vya zimamoto na askari jeshi wanaendelea kufukua vifusi vya jengo hilo lililo maeneo ya Savar, ya jiji la Dhaka. TV zimeonesha wafanyakazi wanawake wakiokolewa wengi wakiwa wamepoteza fahamu. Askari wa zimamoto mmoja amenukuliwa akisema takriban watu 2000 walikuwamo mjengoni wakati linaporomoka
Biashara ya nguo ya Bangladesh imekumbwa na majanga ya moto na ajali zingine kwa miaka kadhaa, licha ya juhudi za kuboresha usalama pahala pa kazi. Mwezi Novemba mwaka jana wafanyakazi 112 walikufa katika mlipuko katika kiwanda cha nguo na kuzua mkanganyiko kwa wafanyabaishara wa kimataifa wa nguo wanaopata bidhaa hiyo Bangladesh.
Afisa mmoja katika chumba cha mikakati ya uokoaji kilichowekwa ili kutoa taarifa kwa watu, alisema watu 96 walikuwa wamethibitishwa kufa na zaidi ya 1000 kujeruhiwa. Madaktari katika hospitali za jirani wamekiri kuzidiwa na majeruhi walioletwa kwao.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Mohammad Asaduzzaman, alisema wamiliki wa viwanda hivyo vya nguo mjengoni humo walidharau onyo la kutoruhusu wafanyakazi mjengoni baada ya nyufa kuonekana katika baadhi ya kuta jana. Katika jengo hilo mlikuwa na viwanda vitano vilivyoajiri zaidi kinamama.