Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya jiji la Dar es salaam limefanikiwa kuwatia mbaroni Watu wawili wanaotuhumiwa kuwa Majambazi waliovamia Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga, jijini Dar es Salaam, huku wengine watatu wakiuwawa katika mapambano ya kutupiana risasi na Polisi katika eneo la Tuangoma, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, tukio hilo la kukamatwa na kuuawa kwa majambazi hao lilitokea Julai 17 mwaka huu maeneo ya Tuangoma. Majambazi wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kinyama la kuuwawa kwa askari wanne na raia watatu katika kituo hicho cha Stakishari wanakadiriwa kuwa kati ya 16 hadi 18.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishina Suleiman Kova amesema kukamatwa kwa majambazi hao inatokana na kikosi kazi kilichoundwa na kanda maalumu kwa kushirikiana na Polisi wa Mkoa wa Pwani.
Kamanda Kova amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao wa ujambazi kulitokana na taarifa pamoja na mtego wa kiintelejensia katika eneo la Tuangoma, ambapo watuhumiwa wakiwa wanakapita katika pikipiki mbili walipowasimamishwa na askari walikaidi amri na kisha kuanza kurusha risasi. Polisi wakajibu mapigo na majambazi watatu wakauwawa.
Majambazi waliouawa ni Abbas Hashimu Mkazi wa Mbagala, Yassin alitambulika kwa jina moja mkazi wa Kitunda Kivule, pamoja Saidi aliyetambulika kwa jina moja mkazi wa Mandimkongo, Mkuranga, mkoa wa Pwani.
Kamanda Kova amesema wanaowashikiria ni Ramadhan Ulatule (15),Mkazi wa Mandimkongo, Mkuranga na Omary Amour( 24) Mkazi Mkazi wa Mbagala Kimbangulile.
Kova amesema baada ya kuwabana watuhumiwa hao wa ujambazi walikwenda kuonyesha bunduki 15 walizopora katika kituo cha Stakishari ambazo walikuwa wamezihifadhi chini ya ardhi bada ya kuweka kinyesi juu yake.
Amesema katika Shimo hilo walikuta bunduki aina Norinko ambayo wanatafuta ilipoibiwa pamoja na fedha taslimu Sh.Milioni 170 za kitanzania.
Aidha amesema jeshi la polisi limejizatiti katika matukio na kutaka watu waachane na biashara hiyo ya ujambazi kwa kuwa huwa hailipi.
Amesema fedha hizo wanazichunguza kujua zimeibwa wapi,na pikipiki mbili aina ya boxer nazo wanazishikiria na kutaka wauza pikipiki kuuzia watu ambao wanavtaarifa nazo.
“Hatutafumbia macho kwa wale askari wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kuwachukulia hatua kali ikiwa hata kama wanajihusiha na ujambazi tutawashughulikia kwani risasi haichagui kuwa huyu raia au askari”amesema Kamishina Kova.
Tukio la kuawawa kwa askari wanne na raia watatu katika kituo cha Stakishari,lilitokea Julai 12, 2015 majira ya saa nne za usiku katika kituo cha Sitakishari.![]()
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujambazi waliovamia kituo cha Polisi cha Stakishari, Tazara, jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari juu ya operesheni iliyofanyika ya kuwakamata watuhumiwa wa ujambazi waliovamia kituo cha Polisi cha Stakishari.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishina Suleiman Kova akionyesha bunduki zilizoporwa katika uvamizi wa uliofanywa na majambazi katika kituo stakishari,Tazara leo jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova akionyesha Fedha taslimu Sh. Milioni 170 zilizokutwa katika Shimo la watuhumiwa wa ujambazi waliovamia kituo cha Polisi cha Stakisaari na kuua askari wanne na raia watatu
Fedha za watuhumiwa wa ujambazi waliovamia kituo cha Polisi cha Stakishali zikiwa katika sanduku zikionyeshwa kwa waandishi wa habari na wananchi leo jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishina Suleiman Kova akionyesha picha za majambazi sugu wanaotafutwa na jeshi la polisi katika wakati akitoa taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa waliovamia kituo cha Polisi cha Stakishari jijini Dar es salaam
Pikipiki zilizokuwa zikitumiwa na watuhumiwa wa ujambazi waliovamia Kituo cha Stakishari zikioneshwa wakati Kamisha Kova wakati akitoa taarifa kukamtwa kwao jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii)