Mkurugenzi wa Hoteli ya Sapphire Court ya Jijini Dar es Salaam, Abdulfatah Salim (kulia) akimkabidhi sehemu ya vifaa vya michezo, Nahodha wa timu ya wamiliki wa Magazeti 'Tando' Blogers Fc, Muhidin Sufiani, ambaye ni mmiliki wa mtanda wa www.sufianimafoto.com, kwa ajili ya kushiriki katika Bonanza maalum la waandishi Medi Day linalofanyika kwenye Viwanja vya Leaders Club Kinondoni kesho. Katikati ni Meneja wa muda wa timu hiyo, Mroki Mroki. Timu hiyo ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza katika michezo na bonanza kama hilo, inatarajia kushiriki katika michezo yote itakayo chezwa hiyo kesho, ikiwa ni pamoja na Soka, Netiboli, Kukimbiza Kuku, Kukimbia na Magunia, Kuvuta Kamba, Kucheza Pool, Kuimba na Kudansi 'Sebene' na mingineyo.
Makabidhiano yakiendelea, hii ni Jezi ya Kipa.
Nahodha wa timu hiyo Sufianimafoto (kushoto) akiwa na Meneja wa muda wa timu hiyo, Mroki Mroki, wakiwa na Vifaa vilivyokabidhiwa.
***************************************
HOTELI ya Sapphire Court iliyopo makutano ya mitaa ya Swahili na Lindi, Dar es Salaam leo imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya wamiliki wa magazeti tando (Blogers FC) kwa ajili ya Bonanza la Media Day, linalotarajiwa kufanyika kesho kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.
Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Sapphire, hoteli iliyojizolea umaarufu mkubwa kwa sasa nchini, Abdulfatah Salim Saleh amesema ameamua kukabidhi vifaa hivyo ili kuunga mkono timu hiyo mpya inayoanzishwa katika tasniya ya michezo nchini.
“Nilipopata ombi lenu, sikutaka hata kujifikiria, nilisema nitawasadia, na huu ni mwanzo tu. Naahidi kushirikiana nanyi zaidi na zaidi na ninawakaribisheni wakati wowote, mimi ni shabiki wa timu yenu kuanzia sasa,”alisema. Kwa upande wake, Meneja wa Muda wa Blogers FC, Mroky Mroky alisema kwamba wanashukuru kwa msaada huo na wanaahidi kudumisha uhusiano mzuri na Sapphire.
“Wazo hili la kuanzisha timu ni la muda mrefu, lakini lilikuwa likisuasua, ila tukaamua kwa vyovyote lazima tutokee kwenye Media Day ya mwaka huu. Tulipofikiria suala la wapi tutapata vifaa vya michezo, vichwa vilituuma kidogo, lakini tunashukuru Sapphier wametuliza maumivu hayo,”alisema Mroky.
Naye Nahodha wa Blogers FC, Muhiddin Sufiani amesema kwamba baada ya kupata vifaa hicyo kesho wanatarajia kuanza kuonyesha cheche zao kesho katika Bonanza la Media Day, lengo likiwa ni kubeba ubingwa upande wa soka na kutwaa pia mataji mengine madogo madogo.
Miongoni mwa wachezaji nyota wanaotarajiwa kuichezea Blogers FC kesho ni Issa Michuzi, Majjid Mjengwa, Sufiani mwenyewe, Majuto Omary, Joseph Lukaza, Shaffi Dauda, Saleh Ally, Mahmoud Zubeiry, Millard Ayo na John Bukuku.
Bonanza la wanahabari linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), litafanyika kesho kwenye viwanja vya Leaders, chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). Pamoja na wanahabari kuchuana katika michezo mbalimbali, lakini Bonanza hilo pia litapambwa na burudani ya bendi ya Extra Bongo na kundi la taarabu la Jahazi Modern.
Kutakuwa pia na mechi maalum baina ya wanahabari ambao wameoa na wale ambao hawajaoa utakaofanyika baada ya michezo ya kawaida baina ya vyombo vya habari kumalizika.
Bonanza litaanza saa tatu asubuhi kwa washiriki kucheza michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, wavu, kuruka kichura, aina mbalimbali za riadha, kuvuta kamba na kucheza muziki. Bonanza litamalizika saa moja usiku.