CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinasikitika kuwajulisha wadau wake kuwa bonanza la wanahabari lililopangwa kufanyika kesho viwanja vya Sigara (TCC) Chang’ombe sasa litafanyika viwanja vya Leaders Klabu, Kinondoni Dar es Salaam siku hiyo hiyo ya Aprili 6,2013.
Uamuzi huo wa kushtukiza umefikiwa kwenye kikao cha dharura kilichofanyika jana usiku kati ya TASWA ambao ni waandaaji na wadhamini wa bonanza hilo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kutokana na kushindwa kuafikiana baadhi ya mambo na menejimenti ya viwanja hivyo.
Tunawaomba sana radhi wanahabari kwa usumbufu mkubwa ambao wataupata kutokana na mabadiliko haya, lakini tunaamini yamefanyika kwa dhamira nzuri yenye nia ya kuboresha bonanza letu na kwa kiasi kikubwa litafana kwa asimilia 100.
Dhamira ya TASWA ni kuona inakuwa na bonanza zuri lisilokuwa na aina yoyote ya kwikwi, hivyo tayari tumeshamalizana na menejimenti ya viwanja vya Leaders Klabu na kila kitu kitakuwa safi kuliko maelezo.
Pia tunaishukuru menejimenti ya viwanja vya Sigara kwa ushirikiano iliotupa kwa nia ya kufanya bonanza hilo eneo lao, ingawa ndoto zetu hazikutumia, lakini tunaamini siku za usoni tunaweza kufanya nao kazi.
Tunasisitiza lengo la bonanza letu ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Awali bonanza letu ilikuwa lifanyike Leaders Klabu, lakini tulilihamishia viwanja vya Sigara kutokana na wadau wengi kuomba wapate nafasi ya kwenda kutazama mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na Barrack Young Controllers ya Liberia kesho. Hata hivyo tunaamini wahariri wa habari za michezo watajipanga vizuri kulingana na mabadiliko hayo na hakuna litakaloharibika.
Pia katika kuboresha bonanza hilo litakalotumbuizwa na bendi ya Extra Bongo na kundi la taarabu la Jahazi Modern, kutafanyika mchezo wa soka kati ya wanahabari ambao wameoa na wale ambao hawajaoa utakaofanyika baada ya michezo ya kawaida baina ya vyombo vya habari kumalizika.
Bonanza litaanza saa tatu asubuhi kwa washiriki kucheza michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, wavu, kuruka kichura, aina mbalimbali za riadha, kuvuta kamba na kucheza muziki. Bonanza litamalizika saa moja usiku.
Ahsanteni.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
05/04/2013