Na Mwandishi Maalum
Hatimaye, Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti Biashara ya Silaha, (ATT) ambao wiki iliyopita ulishindikana kupitishwa kwa kauli moja baada ya Ujumbe wa Syria, Korea ya Kaskazini ( DPRK)na Iran kutia ngumu, umepitishwa na Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa kwa kupigwa kura.
Mkataba huo umepitishwa kwa kura 154 za ndiyo, huku Syria, Iran na Korea ya Kaskazini ( DPRK) zikipiga kura ya hapana na nchi 23 zikapiga kura ya kutofungamana na upande wowote.
Baraza hilo lilihitaji kura 97 tu kuupitisha Mkataba tofauti na wiki iliyopita ambapo wajumbe kutoka nchi 193 walioshiriki majadiliano ya wiki mbili wakati wa MKutano wa Mwisho wa Mkataba wa Silaha walitakiwa kuupitisha kwa kuunga mkono kwa kauli moja badala ya kupiga kura.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya mataifa yaliyopiga kura ya ndiyo, na hasa ikizingatiwa kwamba katika miaka yote ya majadiliano ya kuandaa Mkataba huu, Tanzania imesimama kidete kwa kutaka silaha ndogo na nyepesi ziwe sehemu ya mkataba pamoja na risasi kwa kile ambacho Tanzania imekuwa ikisisitiza kwamba silaha hizo zimekuwa tatizo kubwa na tishio la amani na usalama katika eneo la nchi za Maziwa Makuu.
Baada ya kuona kwamba usiku ule wa Marchi 28, Mkataba ulikuwa umekwama kupitshwa kwa kauli moja, nchi moja ilitoa pendekezo la kutaka liandaliwe Azimio ambalo lingepelekea Mkataba huo uwasilishwe katika Baraza Kuu ili ukaamuliwe kwa kupigiwa kura.
Mkataba utaanza kufanya kazi ndani ya siku 90 baada ya kuwa umeridhiwa kwa sahihi zipatazo 50.
Kupitishwa kwa Mkataba huo kwa kwanza na wa aina yake na Baraza Kuu, kuna andika historia ya aina yake katika Umoja wa Mataifa, na hasa ikizingatiwa kwamba biashara ya silaha ni biashara nyeti na yenye faida kubwa kuliko hata biashara ya madawa ya binadamu.
Lakini pamoja na faida kubwa inayopatika kutokana na biashara hiyo, maisha ya mamilioni ya watu wasiokuwa na hatia yanapotea kila mwaka kutokana na matumizi yasiyo halali ya sihala hasa zile nyepesi na ndogo ndogo.
Dhumuni kuu la Mkatana huu pamoja na mambo mengine ni kusimamia na kuratibu Biashara ya silaha zikiwamo, mizinga ya kivita, magari ya kivita, ndege za kivita, helkpota za mashambuli, meli za kivita, makombora , silaha ndogo na nyepesi.
Aidha Mkataba pamoja na masuala mengine hautaingiali uhuru wa nchi kununua silaha kwa matumizi yake ya ndani na haki ya kujilinda na kulinda mipaka yake, vile vile mkataba hauzui kufanya biashara au kusafirisha aina yoyote ile ya silaha wala kuingilia taratibu ambazo nchi itakuwa tayari imejiweka katika kudhibiti masuala ya silaha.
Inatarajiwa kwamba utekelezaji wa mkataba huu utasaidia sana kudhibiti silaha zisiangukie kwa makundi mbalimbali yakiwamo ya kigaidi na hivyo kujenga na kuimarisha amani na usalama wa jumuiya ya kimataifa.