Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Askari Polisi Nchini wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi ili kuendeleza mahusiano mema na Jamii pamoja na kushirikiana katika kuendeleza mpango wa Polisi jamii na Ulinzi shirikishi ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafichua wahalifu hapa nchini tangu kuanzishwa kwake.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema wakati alipokuwa akizindua Programu za Mafunzo kazini kwa askari Polisi Tanzania nzima katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Jijini Dar es Salaam ambapo uzinduzi huo ulihudhuriwa na Maofisa mbalimbali wa Polisi pamoja na Askari kutoka Makao makuu ya Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam pamoja na Vikosi vilivyopo jijini Dar es Salaam.
IGP Mwema alisema jambo la kutoa huduma bora kwa wananchi siyo la hiari bali ni la lazima hivyo kila askari anapaswa kuboresha huduma anayoitoa kwa kuzingatia mafunzo aliyonayo ili kuleta ufanisi wa kazi na kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Alisema Wananchi nao wanapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi hilo ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka katika kuzuia, kubaini na kutanzua uhalifu hapa Nchini.
“Usalama unaanza na mimi, wewe na sisi sote hivyo kila mmoja anatakiwa ajiulize anachangia nini katika kuimarisha ulinzi wake binafsi, wa jirani yake na wa taifa kwa ujumla kwa vile suala hili siyo la Jeshi la Polisi peke yake ni wajibu wa kila mmoja” Alisema IGP Mwema.
Aidha aliwataka Maofisa na Askari kuitumia vyema fursa ya Mafunzo kazini kujiendeleza kielimu ili kuboresha ufanisi wao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kazi na maisha.
Mwema alitoa wito kwa kila Askari na Ofisa kuutumia vyema mpango huo wa mafunzo kazini kujitengea muda vizuri kwa ajili ya kujisomea nje na saa za kazi ili kuboresha huduma bora kwa wananchi ambapo alisisitiza suala la kutoa huduma bora kwa wananchi siyo la hiari ni kuto na maboresho ya Jeshi la Polisi yanayolenga kufanya kazi kwa weledi na usasa katika kuihudumia jamii na wananchi ..