Mkuu wa Kiengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma akizungumza wakati wa Warsha ya siku tatu kwa wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya Kijamii (BLOGS) hapa nchini kuhusu Wizara hiyo inavyoweza kupeleka habari kwa urahisi kwa wananchi wa kawaida iliyofanyia Kibaha mkoani Pwan,hivi karibuni.
Kutokuwa na utamaduni wa kupenda kusoma vitabu, na taarifa mbali mbali zinazohusiana na maendeleo ya nchi imetajwa kuwa ni kikwazo kikubwa katika mawasiliano kati ya wananchi na taasisi mbali mbali za serikali, jambo ambalo ni hatari katika Taifa linaloendelea.
Kwa mujibu wa utafiti usio rasmi uliofanywa na baadhi ya waandishi wa habri za kijamii nchini, ni asilimia tisa tu ya watanzania, ndio wenye utaratibu wa kupenda kusoma, asilimia iliyobakia, hupata habari kwa njia ya kusikia, ama kwenye vyombo vya habari au kwenye maongezi ya kawaida.
Hii ni moja ya taarifa zilizowasilishwa kwenye warsha ya siku tatu iliyoshirikisha baadhi ya wamiliki wa mitandao ya kijamii na magazeti tando, kwa kushirikiana na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Fedha, katika kujadili jinsi ya kuboresha mawasiliano kati ya wananchi na taasisi za kimaendeleo ili kurahisisha ufikaji wa taarifa za kimaendeleo kwa wananchi.
Kutokana na tabia hii ya kutopenda kusoma, wananchi wengi wamekuwa wakikosa kujua mambo mengi ya kimaendeleo yanayofanyika nchini kwa sababu taarifa hizi mara nyingi huwekwa katika maandishi.
"Limekuwa ni tatizo kubwa sana hapa nchini, watu hawajui kitu na hawataki kujua kwa sababu hawapendi kusoma", alisema wakati akichangia mada mmoja wa washiriki wa Warsha hiyo,Bw. Josephat Lukaza.
Katika Warsha hiyo ya siku ambayo pia ilihudhuriwa na maafisa habari kutoka sekta mbali mbali za kimaendeleo, wadau walikuwa wakitafuta njia mbadala itakayosababisha wananchi kujua mambo mbalimbali ya kimaendeleo ya nchi ili kujua hali halisi ya uchumi wa nchi inavyoendelea.
Naye Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha Wizara ya fedha, Bi Ingiahedi Mduma, alisema ipo haja ya kuwa wabuhifu katika kuhakikisha kwamba kwa njia yoyote ile, tunahakikisha kwamba wananchi wa kawaida, hasa wa vijijini, wanapata taarifa husika kwa wakati muafaka.
Amesema taarifa za kimaendeleo za nchi ni haki ya kila mwananchi kujua na ndio maana sasa wameamua kukaa chini na kuumiza vichwa katika kutaka kujua jinsi ya kuwafikia asilimia kubwa ya wananchi, mijini na vijijini.
Warsha hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro Park Hotel, maeneo ya Misugusugu, wilayani Kibaha, mkoa wa Pwani ambapo pia mikakati mbali mbali ya kimaendeleo ilijadiliwa.
Baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii (Blogs) wakimsikiliza Mkuu wa Kiengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma (hayupo pichani) wakati wa warsha hiyo ya siku tatu
Baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii (Blogs) waliohudhulia Semina hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja.