Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja wachezaji 22 watakaoingia kambini Januari 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma saa 11.30 jioni tayari kwa mazoezi yatakayoanza Januari 7 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally wote kutoka Azam. Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).