Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 115264

TPSF yapongezwa kuimarisha sekta binafsi nchini

$
0
0
 Na Ripota Wetu , Mwanza
 
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imepongezwa kwa jitihada inazochukua hivi sasa kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakua imara, sauti moja na hivyo kuchangia zaidi katika ujenzi wa uchumi.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Mwanza hivi karibuni Bi. Jovita Bubere na Bw. Moses Nyaronga walisema TPSF imesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara zao na kuongeza mitaji.
 
“Tunaomba taasisi hii iendelee na jitihada zake za kuwasaidia wanachama wake mikoani ili kuendelea kutujenga katika kukuza biashara hasa kwa mikutano kama hii ya kikanda kwa nchi nzima” alisema Mama Bubere wakati wa mkutano ulioshirikisha wanachama wa TPSF kanda ya Ziwa.
 
Mama Bubere ambae ni Mwenyekiti wa Asasi ya akina Mama Wajasiriamali Tanzania, yenye makao yake makuu jijini Mwanza wanajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama ususi, ushonaji na utengenezaji wa vifaa vya majumbani.
 
“Tunahitaji msaada mkubwa ilikuweza kufikia malengo yetu,” alisema Mwenyekiti huyo. Akizungumzia soko la Afrika Mashariki, Mwenyekiti huyo alisema wamejipanga vizuri kuingia katika ushindani na tayari wameshaanza kutoa mafunzo kwa baadhi ya akina mama kuhusiana na mbinu za kutumia ushindani unaokuja wa kibiahsra.
 
Kwa upande wake Moses Nyaronga ambae ni Mwenyekiti wa shirika la Lemon Development Foundation lililopo katika wilaya ya Rolya Mkoani Mara, alisema huu ndio wakati wa kuiunga mkono TPSF ili iweze kufanya kazi kwa uhakika zaidi ya ilivyo sasa.
 
“Mikutano ya namna hii ni mizuri, inatuleta pamoja kama wanachama na inasadia kutoa mawazo kwa taasisi hii ili iweze kufanya vizuri zaidi,” alisema Nyaronga. Akizungumzia vijana kukimbilia ajira serikalini, Bw. Nyaronga alisema vijana wengi wanatakiwa kujiunga katika sekta binafsi ambako kwa sasa ndiko kwenye ajira nyingi hasa za kujiajiri.
 
“Sekta binafsi imekuwa sana hapa nchini tofauti na miaka ya nyuma, nashauri vijana wasitegemee ajira serikalini, waingie katika sekta binafsi, kinachohitajika ni kuwezeshwa tu na hili linawezekana kama watajiunga katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali” alisisitiza.
 
“Kuingia katika magenge ya ajabu, kurubuniwa kwenda kwenye maandamano ni ukosefu wa maarifa, na hii inachangiwa na vijana wengi kukosa mwongozo wa nini wachague na nini waache na kwa wakati gani, wakielewa hilo watabadilika,” alisema  Nyaronga.
 
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Geofrey Simbeye, alisema taasisi hiyo ina lengo la  kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wanachama wake katika kuongeza kasi ya uanzishwaji wa makampuni na viwanda kwa ajili ya kuongeza ajira na kuinua uchumi wa nchi.
 
Alisema pia taasisi hiyo inataka kuishawishi serikali kuondoa baadhi ya vikwazo katika ufanyaji biashara ndani na nje ya nchi. Alisema TPSF inataka wanachama wake wafahamiane katika ufanyaji biashara hasa katika mikoa iliyopo katika kanda moja pia kujenga kongano (clusters) imara zitakazoweza kuwaunganisha katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
 
Mkutano huo wa siku moja uliofanyika jijini Mwanza ulikuwa na lengo la kuelimisha na kuhamasisha muundo wa uwakilishi katika kongano (clusters) na kuhusisha mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mwanza, ambayo inaunganisha kanda ya ziwa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 115264

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>