TAMASHA la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Machi 31, mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, linatarajia kuwanufaisha zaidi watu wenye ulemavu, imeelezwa.
Akizungumza jijini leo, Mkurugenzi wa Msama Promotions ambao ndio waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama, alisema kuwa malengo yake kwa mwaka huu ni kuhakikisha tamasha hilo linawasaidia walemavu wengi tofauti na miaka iliyopita.
Msama alisema kuwa nia kuu ya tamasha la mwaka huu ambalo pia litahudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni kuhubiri amani na upendo, lakini nchi haiwezi kuwa na amani na upendo kama kuna baadhi ya watu wanataabika.
“Kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ni amani na upendo, lakini wote tunajua ni ngumu kumuhubiria amani na upendo mtu ambaye anataabika, sasa katika kuhakikisha watanzania wote wanaifurahia amani yao na kuongeza mapendo baina yao, nimepanga kuwasaidia kwa namna yeyote walemavu ili kuwapa nguvu za kuifurahia nchi yao yenye amani,”alisema Msama. Aidha aliongeza kuwa wigo wa kuwasaidia walemavu utaongezeka kulingana na kiasi cha fedha kitakachopatikana.
Tamasha la mwaka huu limeonekana kukubalika na jamii kubwa ya watanzania kutokana na kauli mbiu yake, lakini pia utaratibu wa kuwapa nafasi watanzania kuchagua mikoa na wasanii watakaopamba tamasha umekubalika na wengi hali iliyolifanya tamasha hilo kuwa la watu wote bila kujali dini, rangi ama kabila.
Wanamuziki wa Injili wanaotarajiwa kupamba tamasha hilo ni Sipho Makhabane wa Afrika Kusini, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa ambaye raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi nchini Kenya, pamoja na kwaya ya Ambassadors of Christ yenye makazi yake Kigali nchini Rwanda.
Kwa upande wa wasanii wa hapa nchini watakaotumbuiza ni Upendo Kilahiro, Rose Muhando, Upendo Nkone, John Lissu, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.
Tamasha la Pasaka hilo pia litafanyika katika mikoa ya Mbeya ambapo litaendelea Aprili Mosi kwenye Uwanja wa Sokoine, Aprili 3 litafanyika katika Uwanja wa Samora Iringa na Aprili 6 litakuwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.