Tanzania itakuwa mwenyeji wa Siku ya Kimataifa ya Miti (World Wood Day) ambayo huadhimishwa tarehe 21 Machi kila mwaka. Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Khamis Suedi Kagasheki atakuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo ambayo yatafanyika kwenye Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam.
Siku ya Taifa ya Miti huadhimishwa duniani kote kuhamasisha watu kuhusu manufaa ya miti katika maisha ya kila siku ya binadamu ili waweze kuitunza na kuitumia kiuendelevu.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: Mbinu za kitamaduni za kutumia miti ni nzuri (A cultural approach to achieve wood is good).
Tarehe 21 Machi itakuwa ni siku ya kilele cha maadhimisho hayo ambayo yataadhimishwa kwa siku nne mfululizo tangu tarehe 19 hadi 22 Machi kwa kufanya shughuli mbalimbali zilizopangwa.
Baadhi ya shughuli hizo ambazo zitaanza tarehe 19 Machi katika viwamja vya Karimjee ni:
· Maonyesho ya bidhaa zitokanazo na miti;
· Mashindano ya bidhaa zitokanazo na miti, za hapa nchini na za kutoka nje;
· Kutoa na kujadili mada kuhusu Utamaduni wa Kupenda Miti;
· Kupanda miti katika wilaya ya Kisarawe;
· Kutembelea VETA Chang’ombe;
· Mashindano ya uchoraji kwa watoto.
Maadhimisho haya huratibiwa na Chama cha Kimataifa cha Utamaduni wa Miti (International Wood Culture Society) ambacho kiliasisiwa nchini Marekani mwaka 2007 kwa nia ya kuwatia moyo watu wajenge utamaduni wa kupenda miti.
Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa siku Siku ya Kimataifa ya Miti kwa kuwa imeonyesha juhudi za kuwashirikisha wananchi wake katika kuhifadhi na kupanda miti.
Wananchi wanakaribishwa kuhudhuria mikutano na maonyesho yote yaliyopangwa katika viwanja vya Karimjee maana hakutakuwa na kiingilio chochote.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
17 Machi 2013