Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria katika picha ya pamoja na wadau mmbalimbali na wageni waalikwa baada ya kuzindua kijitabu cha “Mambo 101 Unayohitaji Kuyafahamu Kuhusu Polisi Lakini Unaogopa Kuyauliza. ” Waliokaa kulia kwa Naibu Waziri ni Bi. Benardetha Gambishi, Kamishna wa Haki za Binadamu na kusho ni kwa Naibu Waziri ni Bw. Julian Chandler mwakilishi wa Balozi wa Uingereza nchini.
Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akiinua juu kijitabu cha “Mambo 101 Unayohitaji Kuyafahamu Kuhusu Polisi Lakini Unaogopa Kuyauliza ” kuashhiria kuwa kijitabu hicho kimezinduliwa rasmi. Wanaopiga makofi waliosimama ni Bi. Mary Massey, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kulia kwake ni Mhe. Jaji Kiongozi (Mst.) Amir Manento ambaye ni Mwenyekiti wa Tume hiyo. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Bw. Julian Chandler mwakilishi wa Balozi wa Uingereza nchini.
Mheshimiwa Angellah Kairuki (MB), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akikata utepe katika kuzindua kijitabu cha “Mambo 101 Unayohitaji Kuyafahamu Kuhusu Polisi Lakini Unaogopa Kuyauliza.” Aliyeshika kijitabu hicho ni Bi. Mary Massey, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na kulia kwake ni Mhe. Jaji Kiongozi (Mst.) Amir Manento ambaye ni Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wananchi wametakiwa kutowaogopa na kuwachukia polisi pale wanapokuwa na matatizo yao. Hayo yalisemwa leo na Mhe. Angellah Jasmini Kairuki (Mb) wakati alipokuwa akizindua kijitabu cha mambo 101 unayohitaji kuyafahamu kuhusu polisi lakini unaogopa kuyauliza katika Makao Makuu ya Ofisi za Tume ya Haki za Binadamu (THBUB) jijini Dar-es-salaam.
Mhe. Kairuki alisema kuwa raia wema wenye kuwajibika hawapaswi kuwaogopa na kuwachukia polisi au kuogopa kwenda kituo cha polisi pale wanapokuwa na matatizo au kutoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu. “Wananchi na polisi wanatakiwa wafanye kazi pamoja na kuleta amani na utulivu kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.” Alisema.
Mhe. Kairuki katika uzinduzi huo alisema kuwa ni muhimu kwa wananchi kuzielewa kazi za polisi, jinsi wanavyozifanya na kujua changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao. “Ni ukweli usiopingika kuwa Jeshi la polisi bado linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Naibu Waziri alisema ana amini kuwa kijitabu hiki pamoja na mambo mengine kitasaidia si tu kwa wananchi kujua haki zao bali pia kitakuwa msaada mkubwa kwa askari wa Jeshi hilo katika kujiongezea uelewa na majukumu na mipaka ya kazi zao.
Wakati huohuo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu Bi. Mary Massay alisema kuwa kijitabu hiki kitasaidia kuongeza uelewa wa wananchi watakapokisoma na pia uelewa wa polisi kuhusu wajibu, kusudi, muundo, na haki za wananchi wanapokutana na polisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aliongeza kuwa kijitabu hiki kimeandaliwa chini ya mradi wa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na kazi kazi kwa kushirikiana na Commonwealth Human Rights Initiative yenye makao yake New Delhi nchini India.
Bi. Massay amesema kwa awamu ya kwanza wamechapisha jumla ya nakala 4838, kati ya hizo, nakala 4,500 zimeandaliwa kwa lugha ya Kiswahili, nakala 300 kwa lugha ya kiingereza na nakala 38 zimeandaliwa kwa nukta nundu kwa ajili ya watu wasioona.
Aidha, Katibu huyo wa Tume ya Haki za Binadamu alisema kuwa nakala hizi zitasambazwa bure kwa wananchi na taasisi mbalimbali katika miji ya Dar-es-salaam, Zanzibar, Mwanza na Lindi