Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 115264

SIMBA KIMENUKA

$
0
0

Baada ya vigogo wake wawili hans Poppe na Kaburu kubwaga manyanga, hali imezidi kuwa tete katika Klabu ya Simba baada ya kocha wa timu hiyo Patrick Liewing kuwa mguu ndani mguu nje kutokana na kutolipwa mishahara yake ya miezi miwili ikiwa ni pamoja na kupokonywa gari alilokuwa akilitumia.

Gari alilokuwa anatumia kocha huyo ya GX110 linashikiliwa na uongozi wa hoteli ya Spice, iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam ambao unaidai klabu hiyo kiasi cha Sh. Milioni 28.

Spice ndiyo kambi kuu ya Simba SC mwaka jana, lakini baada ya deni kuwa kubwa, wakahamia katika hoteli ya Sapphire Court, iliyopo Kariakoo pia ambako nako walifukuzwa jana baada ya deni kuwa kubwa. 

Habari zinasema kocha Liewig amekuwa akilalamikia kufanya kazi katika mazingira magumu na hana matumaini ya kutimiza ndoto zake katkka klabu hiyo.

“Nidhamu ya wachezaji ni mbovu, huo ni mtihani mkubwa wa kwanza alionao, bado na matatizo mengine kibao, usimuone vile yule babu, ni mvumilivu sana kwa kweli,”kilisema chanzo chetu kutoka Simba SC.

Tayari benchi la Ufundi la Simba SC nalo limeanza kumeguka, baada ya aliyekuwa Mtunza Vifaa, Kessy Rajab kuandika barua ya kujiuzulu na daktari wa timu hiyo Cosmas Kapinga naye inadaiwa uwenda akaitema timu hiyo.

Jana usiku Basena, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde, wote raia wa Uganda, walifukuzwa kwenye hoteli ya Spice, Kariakoo, Dar es Salaam kutokana na klabu hiyo kulimbikiza deni la Sh. Milioni 27.

Pamoja na kufukuzwa kwa Waganda hao usiku huo, uongozi wa Spice Hotel unashikilia magari mawili ya Simba SC, basi dogo na gari la kocha, aina ya GX110 hadi ulipwe fedha zake.

Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala amesaini hati ya kuahidi kulipa deni hilo baada ya mechi ya leo na kuweka hati yake ya kusafiria kama bondi. Bado Menejimenti ya Sapphire inasistiza kulipwa fedha zake, vinginevyo itachukua hatua za kisheria dhidi ya klabu hiyo.   

Hata hivyo jana uongozi wa Simba kupitia kwa ofisa habari wake Ezekile Kamwaga ulitoa tamko na kudai kuwa uongozi wa Simba, umesikitishwa na hatua ya uongozi wa hoteli a Saphire kwani ilikuwa ni ya gafla sana.

"Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.

"Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.

Alisema Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha hizo.

"Tutakapolipwa fedha hizo, Simba itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.

Alisema Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza na kwamba chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.

"Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili kuongeza mapato yake na tayari awasiliano yameanza na wenzetu wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba nayo ifaidike.

"Simba inaomba pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu kigeni?

"Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Simba ni CREDIT WORTHY INSTITUTION !

Hata hivyo, Kamwaga alisema uongozi wa wekundu hao wa Msimbazi unafikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya jana dhidi ya Coast Union ambapo Simba ilitoka kifua mbele kwa kuinyuka Coast mabao 2-1.

xxxxxxxxxxxxxx

Simba inachukulia kitendo kile kama hujuma na kisheria kinaangukia katika kundi la FORCED IMPRISONMENT  kwa wamiliki kuwazuia watu kinguvu hotelini kwao. WAMILIKI hawakutoa notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya mdomo au maandishi kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Lengo lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo imetoka kulipwa Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita. Uongozi wa Simba SC unaapa kuilinda na kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na maarifa yetu yote.

2. WACHEZAJI, BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA

KUNA taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba wamesimamishwa au kufukuzwa kuchezea Simba. Habari hizi nazo hazina ukweli wowote

Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba umetoa ruksa kwa benchi la ufundi kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi husika. Uongozi hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji wa benchi la ufundi.

Hakuna mchezaji yeyote aliyesimamishwa hadi sasa. Pia uongozi unakanusha taarifa kuwa Daktari Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga, kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina ukweli kwani daktari huyo ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili inayojulikana

Viewing all articles
Browse latest Browse all 115264

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>