ZAIDI ya watoto 30 wanaoishi katika mazingira magumu na yatima wamepelekwa shule za sekondari mbalimbali mjini hapa na Asasi isiyo ya Kiserikali ya TCDA ya mjini Iringa kupitia udhamini wa Fredrick Mwakalebela aliyekuwa mgombea ubunge mwaka 2010
Akizungumza na Ripota wetu Msemaji na Mwanasheria wa Asasi hiyo Daniel Kibiki alisema kwamba Mwakalebela amejitolea kuwasomesha wanafunzi hao walikuwa katika mazingira magumu na yatima walioko katika halmashauri ya manispaa na nje ya mkoa.
Kibiki alisema kwamba malipo ya awali ya shilingi milioni 13.6 zimeshatumika katika malipo ya awali kwa wanafunzi hao katika shule wanazosoma kama malipo ya ada, sare za shule, na matumizi ya kawaida kwa wanafunzi hiyo.
Aidha Kibiki alitoa wito kwa wanafunzi hao mbalimbali kuweza kujitokeza katika asasi hiyo kuweza kupata msaada zaidi wa kimasomo kuliko kuendelea kuzurura mitaani bila kazi na kuongeza kwamba wanafunzi waliopata msaada huo watasomeshwa hadi kidato cha sita kama wakifanya vizuri katkika mitihani yao ya kidato cha nne.
Naye mfadhili wa wanafunzi hao Fredrick Mwakalebela aliwataka wadau mbalimbali kuweza kujitokeza kuwasaidia watoto yatima na wanaoshi katika mazingira magumu kuliko kuendekeza starehe.
“naomba sana mashirika mbalimbali na watu wenye uwezo kujitokeza kuwasaidia watoto hawa kwani kwa sasa wamezidi sana mkoani kwetu”
Mwakalebela alisema kuwa kila mwaka ataongeza idadi ya wanafunzi hasa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kupitia asasi ya TCDA." nitajitahidi kuongeza kila mwaka wanafunzi wenye uhitaji wa elimu ya sekondari na nitawasomesha hadi kidato cha sita hasa kama wakifanya vizuri katika kidato cha nne"
Na Denis Mlowe Iringa.