Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mto Nile ni miongoni mwa mito mikubwa iliyopo upande wa Mashariki ya Bara la Afrika naDuniani kote ukiwa na urefu wa kilomita 6,695 ambapo beseni ya Nile hukusanya maji ya eneo linalojumuisha 10% za eneo la Afrika yote.
Kwa muonekano wa juu Mto Nile unaonekana kama pembetatu wakati upande wa chini wa eneo la Nile (Kaskazini) na upande wa juu (Kusini) kuna mimea mbalimbali inayoota kwa wingi pia katika kipindi cha mwisho wa mwaka eneo la mto Nile huwa linakuwa na mwonekano mwekundu na kuwa na maua yanayojulikana kama lotus flowers.
Japokuwa mimea hii haioti kwa wingi wakati huu kama ilivyokuwa hapo awali, mimea inayoota kwa wingi katika eneo la Mto Nile kwa upande wa chini ni yale yanayojulikana kama Egyptian lotus na kwa upande wa juu hujawa na mimea inayoitwa Cyperus papyrus.
Chemchemi za Nile ni mito yote inayopeleka maji kwenda Ziwa Viktoria katika nchi za Tanzania, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Kenya na kwa upande mwingine wa Nile unaanzia Ethiopia ukiitwa Abbai au Nile ya Buluu unatoka katika Ziwa Tana wakati chanzo cha mbali kabisa ni mto wa Luvironza huko Burundi unaoingia katika mto wa Kagera na kufika Ziwa Viktoria.
Mto huo ambao unaanzia Ziwa Victoria nchini Tanzania, ni chanzo kikubwa cha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani, kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha umeme kwa wakazi wa nchi za bonde hilo.
Kutokana na nchi nyingi kuzungukwa na mto Nile, suala la ushirikiano katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto huo limepewa kipaumbele ili kuzuia migogoro inayoweza kuzuka baina ya nchi ambazo wanatumia mto huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana anasema kuwa azma ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile limepewa kipaumbele na nchi zote zinazozungukwa na mto huo, jambo hilo ndilo limesababisha kuanzishwa kwa Sekretarieti ya NBI mwaka 1999 jijini Dar es Salaam.
“NBI ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile kwa niaba ya nchi wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Misri,” anasema Ntabana.
Kwa upande wa Mratibu wa Kanda wa Kitengo cha Uratibu cha Bonde la Mto Nile (NELSAP-CU), Elicad Nyabeeya anasema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi wanachama kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri ambayo yanapelekea kuinua uchumi wa nchi hizo pia kwa upande mwingine uwepo wa ushirikiano huo umesaidia nchi wanachama kufahamu tamaduni za watu tofauti tofauti.
HABARI ZAIDI BOFYA HAPA