Na Heka Paul na Shakila Galus_MAELEZO –Dar
Wakaguzi wa Ndani wa Serikali wametakiwa kubadilika na kuacha kufanya kazi zao za kila siku kwa kufuata mazoea ili kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Msaidizi wa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Amin Mcharo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya viwango vya kimataifa vya ukaguzi wa ndani kanda ya mashariki.
Alisema kuwa wengi hawapendi mabadiliko na kusema kuwa ni vema kwa watu wa aina hiyo wakaangalia uwezekano wa kutafuta kazi au taalum nyingine ili kutochafua kazi ya ukaguzi.
Mcharo alisema kuwa Ukaguzi wa Ndani ni taalum inayohitaji kwenda na mabadiliko kwa kuzingatia mabadiliko katika miongozo ya kimataifa na inayozingatia uadilifu.
Aliongeza kuwa Tanzania haiwezi kubaki kama kisiwa na hivyo ni vema wakaguzi wake wa ndani wakawa chachu ya utekelezaji wa utendaji wa kazi unaozingatia viwango vya kimataifa vya ukaguzi wa ndani.
Aidha Mcharo alisema kuwa Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali imejipanga kufuatilia kwa karibu utendaji wa Wakaguzi wa Ndani ili kubaini kama utendaji wao unaozingatia maadili ya kazi na ikibainika wanakwenda kinyume na maadili haitasita kuishauri Mamlaka husika kuwaondoa katika nafasi zao.