Deutsche Welle (DW) Idhaa ya Kiswahili inaadhimisha miaka 50 ya idhaa yake ya Kiswahili chini ya maudhui ya “Maarifa na Mwamko“ katika hafla maalumu itakayofanyika jijini Dar es Salaam.
Kwa nusu karne, Deutsche Welle (DW) imekuwa ikitangaza taarifa na habari za uhakika kwa lugha ya Kiswahili kwa ajili ya wasikilizaji kwenye maeneo ya Mashariki mwa Afrika na eneo la Maziwa Makuu.
Tarehe 22 Februari, saa 9.oo mchana katika jengo la Makumbusho ya Taifa, DW itasherehekea maadhimisho haya kwa hafla maalumu jijini Dar es Salaam, Tanzania, ikiwaleta pamoja wachambuzi wanaoheshimika katika mjadala wenye maudhui ya “ Maarifa na Mwamko kupitia Vyombo vya Habari“.
Hotuba maalumu zitatolewa kwa lugha ya Kiingereza na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Klaus-Peter Brandes, na mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt.
“Idadi kubwa ya wasikilizaji wetu wanaishi hapa Tanzania, kwa hivyo lilikuwa chaguo la uhakika kwa ajili ya sherehe zetu,“ alisema Andrea Schmidt. “Kwa miaka 50 iliyopita, DW imejitolea katika utoaji wa habari zenye uwiano na taarifa za uhakika, ikiwapa watu wa Afrika ya Mashariki habari na uchambuzi wa kina juu ya masuala yenye uzito mkubwa.“
Uchambuzi utafanywa na jopo la majadiliano lililotayarishwa kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ofisi ya Dar es Salaam na utafanywa kwa lugha ya Kiswahili. Mohammed Khelef wa DW ataongoza majadiliano hayo akiwa na wataalamu wa vyombo vya habari wanaoheshimika nchini Tanzania, akiwemo Assah Andrew Mwambene (Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo), Mohamed Abdulrahman (DW), Jenerali Ulimwengu (Mwandishi wa habari), Valerie Msoka (Mkurugenzi wa TAMWA) na Maggid Mjengwa (Mtaalamu wa mitandao ya kijamii).
Wahudhuriaji watakuwa pia na fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo na waandishi wa DW kutoka Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania, ambao wanahudhuria hafla hiyo katika jengo la Makumbusho ya Taifa.
Katika kufanya taarifa ziwe na maana Idhaa ya Kiswahili ya DW hutangaza mara tatu kwa siku kwa ajili ya maeneo ya Afrika ya Mashariki na Maziwa Makuu. Ikishirikiana na redio washirika
zinazotangaza kwa masafa ya FM kwenye eneo hilo, DW inaweza kuwapa wasikilizaji habari zenye uwiano juu ya kile kinachoendelea ulimwenguni kwa ujumla na hasa yale yanayoendelea barani Afrika. Ili kupata mtazamo huu wa kimataifa, timu ya waandishi wa habari kutoka mataifa matano ya Kiafrika inafanya kazi na mtandao wa wawakilishi wetu walioko kote Afrika Mashariki na Kati.
Idhaa ya Kiswahili ni moja ya idhaa mashuhuri sana za DW. DW ina kipindi cha kuelimisha kilichoshinda tuzo kadhaa cha “Noa Bongo! Jenga Maisha Yako!“ na makala za aina mbalimbali zinazogusa masuala ya afya, haki za binaadamu, mazingira, wanawake na maendeleo, vijana na mitindo ya maisha na utamaduni.
PRESS: WWW.DW.DE/PRESS
INSIDER BLOG: BLOGS.DW.DE/INSIDER