Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson |
Na Mwandishi Maalum
Wakati viongozi wakuu mbalimbali nchini Tanzania wakisisitiza haja na umuhimu wa viongozi wa madhebu ya dini kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara. Umoja wa Mataifa nao kwa upande wake unaeleza kwamba ni kwa njia ya mazungumzo migogoro ya dini inaweza kuepukika.
Kauli hiyo ya Umoja wa Mataifa, umetolewa na Jan Eliasson,Nabu Katibu Mkuu wa chombo hicho ya kimataifa , wakati wa tukio maalum la Muungano kwaajili ya utamaduni wa Amani kwa njia ya maelewano ya madhehebu ya dini. Tukio ambalo limefanyika mwishoni mwa wiki hapa umoja wa mataifa likiwahusisha wawakilishi kutoka dini mbalimbali, vyama visivyo vya kiserikali na mabalozi.
“Migogoro mingi inayoendelea hivi sasa duniani, ni migogoro ya kidini. Mazungumzo baina ya imani mbalimbali yanaweza kusaidia kusuluhisha migogoro hii. Tunaweza kupambana na chuki kwa njia ya mazungumzo ili kujenga maelewano na kujenga daraja la maisha bora kwa jamii zetu”.Akasema Naibu Katibu Mkuu
Na kuongeza kuwa, dini zote zimekuwa mstari wa mbele katika juhudi si tu za kuhimiza amani na upendo, bali hata katika miradi ya kuwasaidia watu maskini kwa kutoa huduma kama vile za afya, na kuwasaidia vijana.
Hata hivyo akaonya kwamba, siasa kali za kidini zimekuwa chimbuko la uharibifu wa kudumu na mateso katika jamii.
Na kwa sababu hiyo akasisitiza kutoachiwa kwa vikundi vya dini vyenye misimamo mikali kuharibu na kuvuruga amani na maendeleo na kazi nzuri inayofanywa na madhehebu ya dini .
“Hatuwezi kuruhusu kundi dogo la watu wenye misimamo mikali kuharibu kazi nzuri zinazofanywa na jumuia za kidini kwa waumini wao duniani kote” akahimiza Bw. Eliasson
Akaelezea wasi wasi wake kuhusu vijana kutumiwa na vikundi vyenye misimamo mikali kueneza kampeni za chuki na vurugu kwa ahadi za kupata dhawabu au wokovu ili wao watimize malengo yao.
“Kwa kawaida vijana wana nguvu. Tunapashwa kutafuta njia nzuri na sahihi za kuwafanya wazitumie nvugu zao kuboresha maisha yao” akasisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Vuk Jeremic kwa upande wake alisema Umoja wa Mataifa unaweza kufaidika sana kama viongozi wote wa dini watajihusisha na kufanya kazi kwa moja ili kuleta amani. Huku akiutaka Umoja huo kuogeza kasi ya kushirikiana na madhehebu ya dini.
“ Hebu basi na turejee na kukumbatia wito unaotolewa na imani zetu, wito wa kuwasaidia watu wengine wenye matatizo, wito wa kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe,ikiwa ni pamoja na uhuru wa kuabudu wakati wowote na mahali popote bila ya kujali tofauti zetu za imani”.
Rais huyo wa Baraza Kuu akasema kila mtu anawajibu wa kuwasiliana na mwenzake na kusahau yaliyopitia na kuonya kwamba kama vyanzo vilivyopita vya migogoro ya kidini vitaendelea kukumbushiwa mara kwa mara, kuna hatari kubwa ya kuitumbukiza dunia katika machafuko ya kutisha.