Na Freddy Macha
Maonyesho maarufu ya mavazi ya kimataifa –London Fashion Week- yatamega kitengo chake cha kimataifa kusaidia kutangaza kazi za washoni wapya toka Tanzania ndani ya Ubalozi wetu leo Ijumaa mjini London.
Mada ya maonyesho haya yatakayoendelea kwa juma zima ni “Swahili Flavour” (Ladha ya Kiswahili). Yategemea kutukuza kazi za Watanzania kupitia wabunifu mavazi Christine Mhando (anayetumia jina la ubunifu: “Chichia London”) na Anna Lukindo ( “Anna Luks”).
Christine Mhando alihitimu chuo cha Usanii cha Kent mwaka 2002 na huhimiza mtindo wa Kanga kama wajihi wa kazi zake, ilhali Anna Luks aliyemaliza chuo cha Middlesex, London hutumia fani inayosisitiza kamba kamba, mavazi ya kike kwa dunia ya kisasa.
Wote wanasema wana lengo la kukuuza sanaa na ubunifu, utamaduni wa Kitanzania, kutangaza taswira za Kiswahili na sura mbalimbali za Afrika Mashariki.
Pamoja nao wasanii hawa ni msaidizi wao–ambaye bado anasomea upambaji mavazi, Margaret Waiyego - mzawa wa Kenya. Kaimu Balozi wa Tanzania, Mheshimiwa Chabaka Kilumanga alisema jana kwamba maonyesho haya ya kimataifa yatakua nafasi kubwa kwa Tanzania kujenga jina lake na ni sehemu mahsusi ya kujivunia utamaduni wetu.
Shirika la maendeleo ya utamaduni na elimu British Council ndiye mgharamiaji wa shughuli hii yenye lengo la kujenga vipaji na kazi za mavazi za washoni wasiofahamika duniani.
Tovuti: www.freddymacha.com
1. Anna Lukindo(Anna Luks) akiwa kazini kutayarisha ufunguzi huu jana
1. Mlango wa kuingilia maonyesho umeshatayarishwa
Moja ya matumizi mbalimbali ya kanga kama foronya za mito katika kochi
Msaidizi akiwa kazini kusaidia matayarisho haya