Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kifungo cha miaka tatu jela mtu aliyedaiwa kumuibia Sh milioni 37 Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi.
Mshitakiwa huyo ni Abdallah Mzombe ambaye amehukumiwa baada ya kumkuta na hatia. Mbali ya adhabu hiyo, Mahakama imeamuru mshitakiwa kulipa fedha hizo wakati akitumikia kifungo hicho.
Hakimu Genvitus Dudu alitoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao ulikuwa na mashahidi saba.
Mshitakiwa huyo alikuwa anadaiwa kuiba fedha hizo baada ya kuaminiwa na Mwinyi kusimamia na kukusanya kodi ya nyumba zake mbili zilizopo Mikocheni B na Msasani jijini Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Dudu alisema, mshitakiwa amepatika na hatia ya makosa mawili ya wizi wa kuaminiwa,na anahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa lakini atatumikia vifungo hivyo kwa wakati mmoja ambapo ni sawa na miaka mitatu.
kwa mujibu wa ushahidi mshitakiwa haibishaniwi alikuwa wakala wa kukusanya kodi katika nyumba za Mwinyi na alipokea fedha za kodi kutoka kwa wapangaji.
Katika makubaliano yao Mwinyi alimwambia Mzombe akipokea kodi, fedha nyingine afanye ukarabati wa nyumba hizo na nyingine fedha zinazobaki ampelekee lakini mshitakiwa hakufanya hivyo badala yake alizitumia kwa matumizi yake binafsi.