Joseph Ngilisho,Arusha
WANAWAKE wawili wanandugu wameuawa kinyama katika nyumba waliokuwa wakiishi na watu wasiojulikana na miili yao kukutwa baada ya siku tatu ikiwa imelaliana huku ikiwa imeharibika vibaya.
Kugundulika kwa miili hiyo kumetokea leo majira ya saa 3.15 katika eneo la daraja mbili manipsaa ya jiji ya Arusha baada ya majirani kuhisi harufu kali iliyokuwa ikitokea ndani ya chumba hicho walichokuwa wamepanga katika nyumba inayomilikiwa na merehemu Samson Kivuyo.
Taarifa zimeeleza kuwa majirani hao walijikusanya na kutoa taarifa kwa uongozi wa eneo hilo ambao kwa pamoja walikubaliana kutoa taarifa polisi ambapo ,polisi walifika eneo la tukio na kuvunja mlango ,ndipo walipokuta miili ya marehemu hao ikiwa imeharibika vibaya.
Miiili ya marehemu hao ilikutwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili, huku ndani ya chumba hicho kukiwa kimevurugika na baadhi ya vitu kuvunjika hali ambayo inaaminika kwamba kabla ya mauaji hayo kulikuwa na mvutano wa kutoelewana.
Akizungumza na vyombo vya habari msimamizi wa nyumba hiyo,Fatina Mringo aliwataja marehemu hao kuwa ni,Zainabu Iddy(Zai) mwenye umri wa miaka 19 na Zena Sadick Shengwatu mwenye umri wa miaka 40 ambaye alikuwa mfanyabiashara wa nguo na mmiliki wa chumba hicho.
Alieleza kuwa siku ya jumamosi marehemu hao walionekana majira ya mchana wakiwa nyumbani, na marehemu Zena alikabidhiwa fedha na wapangaji wenzake na kwenda kulipia bili ya umeme Tanesco na baadae alirudi na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
Hata hivyo habari zimedai kwamba marehemu hao kwa pamoja hawakuweza kuonekana tena hadi miili yao ilipokutwa chumbani ikiwa imeharibika vibaya na kutoa harufu kali.
Hata hivyo baadhi ya majirani wakielezea tukio hilo wamebainisha kwamba marehemu hao mara nyingi walionekana kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume tofauti na kwamba siku ya tukio Zena alionekana akichukuliwa na gari dogo aina ya teksi huku gari jingine lilionekana likingia nyumbani kwake.
Majirani hao wamedai kwamba marehemu hao ambao ni wakazi wa Lushoto mkoani Tanga waliishi katika nyumba hiyo katika mazingira ya kutokuwa na waume .
Kamanda wa polisi mkoani Arusha Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba uchunguzi unaendelea na kwamba hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa Mount Meru kwa uchunguzi wa daktari.