MWENYEKITI wa kamati ya kuratibu Tamasha la kila mwaka la Pasaka, Alex Msama, amesema tukio hilo linalohusisha onyesho la muziki wa Injili kutoka ndani na nje ya nchi, ni la kila mtu kwani litaendelea kusaidia makundi mbalimbali yasiyojiweza na walemavu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msama alisema ingawa wao ni waratibu, lakini lengo hasa la tamasha hilo ni kupata kiasi cha fedha za kuwapatia watu wanaohitaji msaada, kama vile watoto yatima, walemavu wa aina mbalimbali na wale wanaokumbwa na majanga makubwa. “Hili ni tamasha lao, wao ndiyo wadau wakubwa kwa sababu wananufaika nalo. Kila mtu ni shahidi kuwa tumekuwa tukitoa misaada ya aina mbalimbali kwa makundi maalum ya watu.
Hata hivyo, ni vyema pia tukaweka wazi kuwa wanaowezesha haya yote ni watu wanaokuja kuunga mkono tukio hili linalofanyika kila mwaka,” alisema Msama. Kuhusu tamasha la mwaka huu, Msama alisema hawezi kulizungumzia kwa undani kwa sasa kwa vile bado wanaendelea na taratibu za kupata kibali chake na wakishafanikisha suala hilo, wataweka wazi kwa umma ili ujue. Katika tamasha la mwaka jana lililofanyika kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, waimbaji mbalimbali maarufu walipanda jukwaani na kutoa burudani safi.
Miongoni mwao walikuwa ni Rose Mhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival. Waimbaji wan je walioshiriki tamasha hilo ni pamoja na Rebeca Malope wa Afrika Kusini, Maryanne Tutuma, Solomon Mukubwa na Anastazia Mukabwa (Kenya), Faraja Ntaboba (Congo) na Ephraim Sekeleti.