Na Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulio lililofanywa dhidi ya walinda Amani wa Tanzania katika UNAMID, na limetaka uchunguzi wa kina ufanyike.
Taarifa ya Baraza hilo ambalo ndilo lenye dhamana Kuu ya usimamizi wa Amani ya kimataifa na jukumu la kuidhinisha Misheni zote za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, imetolewa kwa niaba ya Baraza na Marekani ambaye ni Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Julai.
Taarifa inasema, Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama wanalaani kwa nguvu zao zote mashambulizi yaliyofanyika Julai 13 na watu wasiojulikana dhidi ya walinzi wa Amani wa UNAMID huko Darfur, waliokuwa katika doria katika eneo la Magharibi ya Nyala Kusini mwa Darfur na kusababisha vifo vya walinzi wa Amani Saba , majeruhi 17, akiwamo Polisi huku hali za majeruhi wawili kati yao ikielezwa kuwa ni mbaya.
Wajumbe wa Baraza la Usalama Kuu wanatoa salamu zao za rambirambi kwa familia za walinzi hao wa Amani waliopoteza maisha katika shambuli hilo, na pia kwa Serikali ya Tanzania na kwa UNAMID.
Baraza Kuu la Usalama limeitaka Serikali ya Sudan kufanya uchunguzi wa kina juu na tukio hilo na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wale wote waliohusika.
Taarifa hiyo inaeleza zaidi kwamba. Baraza Kuu la Usalama , limeonyesha wasiwasi wake kuhusu mazingira ya shambulio hilo, moja ya shambulio baya kuwahi kufanyika dhidi ya walinzi wa UNAMID tangu kuanzishwa kwake.
Baraza Kuu la Usalama katika taarifa yake hiyo limesisitiza kwamba shambulio au vitisho vya aina yoyote dhidi ya UNAMID havikubaliki. Na limetaka kutojirudia tena kwa tukio kama hilo.
Vile vile Baraza Kuu la Usalama limerejea msimamo wake kwamba linaunga mkono kwa kauli moja Misheni ya kulinda Amani ya UNAMID na limetoa wito kwa pande zote huko Darfur kushirikiana na Misheni hiyo.
Wakati huo huo, kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amekuwa akipokea kwa niaba ya serikali na familia, salamu za pole kutoka kwa Mabalozi wenzake.