Mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Christine Ishengoma akifungua kikao cha RCC mkoa wa Iringa kulia ni mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi na kushoto ni katibu tawala mkoa wa Iringa Wamoja Ayub.
Wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri mkoa (RCC) wakiwa wamesimama kwa kumkumbuka aliyekuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo marehemu Mohamed Gwalima aliyefariki ghafla hivi karibuni ,kutoka kushoto ni mkuu wa wilaya ya Kilolo Gerald Guninita, mbunge wa jimbo la Kilolo Prof Peter Msolla,mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo Joseph Muhumba na kaimu mkurugenzi wa wilaya ya Kilolo.
Wajumbe wa kikao cha RCC Iringa wakimkumbuka aliyekuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilolo Mohamed Gwalima aliyefariki dunia hivi karibuni ,kutoka kulia ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati, mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Lediana Mafulu Mng'ong'o ,mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini Mendlad Kigolla ,mku wa wilaya ya Mufindi, Evarita kalalu na mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi Peter Tweve .
Na FrancisGodwin blog -mzee wa matukiodaima
Mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Christine Ishengoma ameziagiza Halmashauri mkoa wa Iringa kuhakikisha wanasimamia vema fedha za miradi zinazotolewa na serikali katika maeneo yao.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo leo katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC).
Amesema kuwa lengo la serikali kutuma fedha za miradi katika Halmashauri husika ni kuwezesha kusukuma mbele kasi ya miradi ya maendeleo katika Halmashauri.
Hivyo alisema haitapendeza kuona fedha za miradi katika Halmashauri zinakosa usimamizi mzuri na kupelekea miradi kukwama kumalizika kwa wakati.
Aidha alitaka viongozi wa Halmashauri kubuni miradi ya kuziwezesha Halmashauri zao kuongeza mapato zaidi. Kwani alisema bila ya Halmashauri kubuni miradi ya kiuchumi uwezekano wa Halmashauri kujiendesha utakuwa mdogo zaidi. Kuhusu watumishi wasiojituma katika kazi mkuu wa mkoa ametoa onyo kwa watumishi hao na kuwa kamwe hata wavumilia.
Katika hatua nyingine mkuu huyu wa mkoa ametoa agizo kwa jeshi la polisi mkoa wa Iringa kupitia askari wake wa usalama barabarani kuwakamata na kuyakamata na kuyatoza fani magari yote ya abiria ambayo yatapita katika mkoa wa Iringa bila kuwa na vifaa vya kuhifadhia taka na yale yatakayobainika yakichafua mazingira ovyo.