Mahakimu Mkoani Lindi wametahadharishwa kutojiwekea malengo makubwa ya kutaka kujipatia utajiri wa haraka haraka tofauti na vipato vya mishahara yao ili kujiepusha na uwezekano wa kujitumbukiza kwenye vitendo viovu vya kuomba rushwa na hivyo kupindisha maamuzi ya utoaji haki kwa jamii ikiwemo wanyonge kutokuwa na haki.
Taadhari hiyo imetolewa na katibu msaidizi idara ya viongozi wa utumishi wa umma/siasa Bi Zahara Guga kwenye mafunzo ya kuwaaelimisha mahakimu Mkoani humo juu ya kusimamia utoaji wa haki kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kuwatendea haki wananchi.
Aidha Bi Zahara Ameonya kuwa kama utoaji haki kwa wananchi usipofanywa kwa umakini na uadilifu mkubwa, kuna hatari kwa mahakimu hao wakawa chanzo cha kulisababishia taifa kuingia kwenye migogoro na hatimaye uvunjifu wa amani usio wa lazima.
Akifungua Mafunzo hayo,Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Lindi,Joh Likango alitaja baadhi ya mapungufu na matatizo ya kimaadili kwa Mahakimu ni pamoja na rushwa , utoaji wa huduma usioridhisha, matumizi mabaya ya madaraka, wizi, unyanyasaji wa kijinsia pamoja na rushwa ya ngono.
Likango alisisitiza kuwa Rushwa Imekuwa kero kubwa kwa jamii kutokana na kukithiri kwenye sekta za umma jambo ambalo linawafanya wananchi kununua haki zao na kusababisha huduma nyingi za kijamii kutolewa chini ya kiwango.
‘mahakama ni chombo ambacho kinatoa haki kwa jamii bila ya upendeleo hivyo basi idara hiyo inawajibu kutekeleza majukumu yake kuhudumia wananchi bila ya upendeleo ili Haki itolewe bila Chochote chenye kushawishi vinginevyo Mtapoteza Amani iliyopo”Alimalizia Likango.
Kwa upande wake Hakimu Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Dunstan Ndunguru kwa niaba ya wenzake amewataka mahakimu wenzake kuyatumia mafunzo hayo kurekebisha kasoro zao ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki wanayostahili pale wanapohitaji msaada wa kisheria.
Jengo la Mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi Lindi
Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Lindi akifungua mafunzo kwa mahakimu wa mkoa wa Lindi kuhusiana na Maadili.
Mahakimu toka mahakama za mkoa wa Lindi wakiwa katika mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na Sekriterieti ya maadili ya Umma na kufanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi,John Likango,wa pili toka kushoto waliosimama akiwa katika Picha ya Pamoja na mahakimu wa mahakama za mkoa wa Lindi wakiwemo maafisa toka Sekriterieti ya maadili ya Umma.Picha na Habari zimeleta na Abdulaziz Video,Globu ya Jamii-Lindi.