Rais wa Benin ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA), Mhe. Boni Yayi anatarajiwa kuwasili hapa nchini tarehe 15 Januari, 2013 saa 2.00 usiku kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Yayi atapokelewa na Mwenyeji wake Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiwa nchini Mhe. Yayi anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam tarehe 16 Januari, 2013. Mbali na kuzungumzia masuala ya ushirikiano kuhusu nchi hizi mbili, viongozi hao watazungumzia masuala muhimu kuhusu Bara la Afrika.
Mhe. Yayi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wakati wa Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi wa Umoja huo uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi Januari 2012 na atamaliza muda wake wa uenyekiti wakati wa Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Umoja huo utakaofanyika pia Addis Ababa tarehe 27 na 28 Januari 2013.
Mhe. Yayi anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 16 Januari 2013.
Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam.
14 Januari, 2013.