Wakulima wa zabibu Mkoani Dodoma wametakiwa kutambua kuwa zao la zabibu lina thamani ya kimataifa na siyo ya kimkoa wala kitaifa na hivyo bei yake inatakiwa kuwa ya kimataifa kulingana na masoko ya kimataifa.
Wakulima hao wameshauriwa wasikubali mtu yeyote awapangie bei ya zabibu kimkoa au kitaifa kwa kuwa bei ya zabibu ya hapa nchini inatakiwa kushabihiana na kushindana na bei ya zabibu inayolimwa na kuuzwa kwenye nchi nyingine Duniani kama vile Afrika kusini na Italia.
Ushauri huu ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa zao la zabibu kilichofanyika mjini Dodoma ambapo kiliwajumuisha wakulima wa zabibu kutoka vijiji vinavyolima zabibu hapa Mkoani Dodoma.
Wadau wengine walikuwa umoja wa wafanyabiashara, wakulima na wenyeviwanda TCCIA, Bank ya NMB, Wataalamu wa masuala ya Ushirika kutoka Idara ya Ushirika na Maafisa kilimo wa Wilaya zinazolima zabibu.
Ushauri huo umetolewa kufuatia kuwepo kwa malalamiko ya wakulima kuonewa, kunyanyaswa na kuhujumiwa hasa kwenye soko la zabibu na baadhi ya wanunuzi kwa bei isiyolingana na hadhi ya kimataifa ya zao la zabibu wakati wanunuzi wenyewe wanauza zabibu hizo kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi kwa bei kubwa hadi kufikia zaidi ya mara sita ya bei wanayonunua kwa wakulima.
Dr. Nchimbi alifafanua kuwa kwa Mkoa wa Dodoma, zao la zabibu ni mojawapo kati ya mazao ya msingi, nguzo na mhimili kwa maendeleo ya Mkoa na Taifa, hivyo ni lazima lilindwe kwa masoko na bei za uhakika. Wataalamu wasaidie kutengenezwa na kupatikana kwa bei na masoko hayo. Vilevile Dr. Nchimbi aliwaagiza Halmashauri za Wilaya Mkoani Dodoma na CDA kuhakikisha wanakuwa na mpango kabambe wa miradi na mashamba ya zabibu na kuhakikisha wanayatolea hati miliki.
Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa wakulima wa zabibu Mkoa wa Dodoma (DOGCO Ltd) ndugu Omary Ramadhani alisema kwa sasa umoja huo unaundwa na AMCOS sita na bado wakulima kwenye vyama vyao vya msingi wanaendelea kujiunga.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa Agenda za Msingi zilizopo mezani kwa DOGCO ltd kwa sasa ni pamoja na uanzishaji wa kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la zabibu na kusindika mchuzi wa zabibu na tayari wameshafanya mazungumzo na na Benki ya Uwekezaji TIB.
Vilevile ni pamoja na kujadili juu ya upatikanaji wa bei elekezi ya zabibu kitaifa ambayo wanapendekeza serikali itangaze bei hiyo kama ilivyo bei ya mazao mengine kama kahawa, chai, korosho, pamba na tumbaku.