Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa ambaye yuko nchini kuhudhuria Mkutano wa Global Smart Partneship jana alitembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuvutiwa na mandhari nzuri ya Serengeti iliyosheheni wanyama mbalimbali. Rais Rajapaksa aliwasili asubuhi jana na kufanya safari ya utalii wa siku (day trip) akiwa amefuatana na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki. Katika muda mfupi aliotembelea Serengeti aliweza kujionea wanyama mbali mbali kama vile Simba, Tembo, Twiga na makundi makubwa ya pundamilia na nyumbu.
Aidha, kufuatia kuvutiwa na uzuri wa Serengeti Rais Rajapaksa aliahidi kutembelea tena hifadhi hiyo mwezi ujao akiwa na familia yake ili waweze kujionea uzuri wa hifadhi hiyo akiwa na muda wa kutosha pamoja na familia yake.
Rais Mahinda Rajapaksa (katikati) akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki (kulia) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Butiama Anjelina Mabula mara baada ya kuwasili katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Rais Mahinda Rajapaksa akiaga mara baada ya kutembelea Hifadhi ya Serengeti tayari kwa safari ya kurejea Dar es Salaam.