Imeandikwa kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy Macha
Mara ya mwisho Tanzania kusikika kimataifa michezoni ilikuwa 1980 wakimbiaji Filbert Bayi na Suleiman Nyambui walipotwaa medali za Olimpiki, Moscow na timu yetu ya taifa ya mpira iliposhiriki fainali za kombe la Afrika mjini Lagos , Nigeria...
Watoto wadogo wakisakata gozi Academy of Light. Samaki mkunje angali mbichi... Kiu ya miaka 30 imezungumziwa na kujadiliwa sana hatimaye tumeanza kuzoea kushangilia wengine. Tumezoea mtazamo huu kiasi ambacho ni rahisi kwa shabiki wa Kitanzania kuijua timu nzima ya wachezaji wa Manchester United au Barcelona kuliko Yanga na Simba. Kati ya sababu kuu za kushindwa huku kila mwaka ni kutowekezea katika matayarisho na kutochangamkia tulicho nacho. Wenzetu wa Hispania, Brazil, Uingereza, Nigeria, Ivory Coast, Kenya nk wanatuzidi moja. Wanajipenda.
Rais akionyeshwa ramani ya mpango wa chuo cha mpira kitakachojengwa Dar es Salaam. Sisi (kama hawa wenzetu) tunao wachezaji wenye vipaji. Tunao pia uchungu kwa nchi yetu; na kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete alipoitembelea klabu ya Sunderland AFC Jumapili 16 , Juni, “Watanzania tunapenda michezo.”
Mheshimiwa Rais mwenyewe, aliwaeleza wanahabari waliomhoji kwamba zamani alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu. Ni vizuri kuwa na kiongozi mpenda michezo. Na mwaliko Rais aliopewa na mwenyekiti wa klabu ya Sunderland AFC , Ellis Short umeotesha si tu mbegu ; sharti tuanze kuchangamkia tulicho nacho. Mpenda kwao hutunzwa. Jamani, eh, tuichangamkie dili. Dili yenyewe ni ipi?
Rais Kikwete akitembezwa viwanja vya Academy of Light. Mkono wake wa kushoto ni Mkurugenzi wa Biashara klabu ya Sunderland AFC, Gary Hutchinson na kulia kwake, Profesa Anna Tubaijuka, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Rais na msafara wake uliomhusisha pia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara, walielezwa kuwa kampuni ya kimataifa ya umeme –Symbion Power- itaanza mara moja kujenga chuo (Sports Academy) cha kufundishia mpira jijini Dar es Salaam. Afisa Mkuu wa Symbion, Bw. Paul Hinks alisema punde ujenzi utakapomalizika, Sunderland AFC itaanza utaalamu na uzoefu wake kwa kutoa mafunzo ya mchezo huu unaopendwa Tanzania. Kazi hii ina hatua mbili. Ya kwanza Dar es Salaam, ya pili, kujenga na kuendeleza mpira Tanzania ili kuufikisha hatua ya juu, aliahidi Hinks.