Spika wa Bunge la Oman (Majlis) Mhe. Sheikh Khalid Al Maawal na Ujumbe wake watafanya ziara ya kikazi ya siku sita hapa Nchini kuanzaia kesho Juni 25, 2013 kufuatia mwaliko rasmi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda uliotolewa kwa niaba yake na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge walipotembelea Oman Mwezi Februari Mwaka huu.
Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika wakati wa ziara yake hapa Nchini ni uzinduzi rasmi wa Chama cha Urafiki wa Kibunge baina ya Oman na Tanzania (Oman - Tanzania Parliamentary Friendship Group); siku ya tarehe 27 Juni, 2013 katika wa Pius Ukumbi wa Msekwa, Bungeni Dodoma. Hii itakuwa hatua muhimu ya Kuanzisha ushirikiano wa moja kwa moja baina ya Mabunge hayo mawili.
Spika huyo wa Oman anatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda, kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Kamati ya Uongozi ya Bunge na Tume ya Utumishi wa Bunge. Aidha anatarajia kuwa na mazungumzo rasmi na uongozi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam akiwa Dodoma
Mhe. Sheikh Al Maawal atafanya pia ziara katika Chuo cha Dodoma na kutembelea Jimbo la Kongwa kabla ya kuelekea Arusha ambako atatembelea vivutio vya kitalii vya Ngorongoro na Serengeti. Pamoja na kutembelea vivutio hivyo, Mhe. Sheik Maawal atatembelea pia kisiwa cha Zanzibar ambako atakutana na Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Seif Ali Idd, na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho kabla ya kurejea Oman akitokea Zanzibar tarehe 3 Julai, 2013.
Imetolewa na Idara ya:
Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa.
Ofisi ya Bunge
DODOMA
25, Juni, 2013