WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wakazi wa kata ya Mnacho, wilayani Ruangwa kwenye mazishi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Bw. Daniel Mtawa ambaye alifariki dunia Mei 7, 2017.
Akizungumza na waombolezaji katika ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye kijiji cha Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi jana (Jumatatu, Mei 8, 2017), Waziri Mkuu alisema msiba uliowapata wana-Mnacho ni mkubwa, na akatumia fursa hiyo kuwapa pole wanafamilia na wanakijiji wenzake.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, anatoka katika kijiji cha Nandagala, kwenye kata hiyohiyo ya Mnacho.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi ambazo zilitolewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. “Mheshimiwa Rais ametoa salamu za pole kwa mke wa marehemu, familia na wana-Ruangwa wote. Pia Mheshimiwa Makamu wa Rais, anawapa pole wana-Ruangwa wote kwa msiba huu mzito,” aliongeza.
“Ndugu yetu Mtawa amemaliza safari yake na ametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumuombea marehemu Mtawa, kila mtu kwa imani yake. Ninatoa pole kwa familia, kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na madiwani wenzangu wote,” alisema.
Akitoa salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Bw. Rashid Nakumbya, alisema Bw. Mtawa alikuwa diwani wa kata hiyo tangu mwaka 2015 lakini alianza kupata tatizo la shinikizo la damu Desemba mwaka jana. “Alilazwa katika hospitali ya Nyangao kwa mwezi mmoja, na baadaye akahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kwa miezi miwili kabla ya kupata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani kuendelea na dawa,” alisema.
Marehemu Mtawa ameacha mjane, watoto saba (wa kiume watano na wa kike wawili) na wajukuu wanane.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mbunge wa Ruangwa, akiweka mchanga kwenye kaburi la aliyekuwa Diwani wa CCM Kata ya Mnacho ,Kijij cha Nandagala , Bw. Daniel Petro Mtawa ambaye amefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa kijijini kwake Nandagala Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi May 8 ,2017. (PICHA NA OWM)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa salamu za Pole Katika Msiba kwa aliyekuwa Diwani wa CCM Kata ya Mnacho ,Kijij cha Nandagala , Bw. Daniel Petro Mtawa aliyefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa kijijini kwake Nandagala Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi May 8 ,2017. (PICHA NA OWM)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ameongozana na Viongozi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara pamoja na wananchi kuelekea makaburini kwa ajili ya mazishi ya aliyekuwa Diwani wa CCM Kata ya Mnacho, Kijiji cha Nandagala , Bw. Daniel Petro Mtawa aliyefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa kijijini kwake Nandagala Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi May 8,2017. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego na wa pili kulia, ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa , Bi. Rukia Mhango. (PICHA NA OWM)
KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA