Na Catherine Sungura, WAMJW
Ujumbe wa wawekezaji toka nchini Misri umewasili nchini kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania kwa nia ya kujenga viwanda vya dawa za binadamu zikiwemo za majimaji pamoja na zile za antibiotic.
Ujumbe huo ulikutana jana na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na wawakilishi toka wizara Viwanda,Biashara na Uwekezaji na Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) kwenye ofisi ndogo ya wizara ya afya, maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto iliyopo jijini Dar es Salaam
Ujumbe huo ulisema kuwa kiwanda walichokusudia kujenga nchini hapa kitazalisha dawa za majimaji yaani “IV Fluids” pamoja na “antiobiotics” za aina mbalimbali ikiwemo "Paracetamol IV” na dawa za kutibu Malaria
Aidha, walisema lengo lao ni kujenga kiwanda kikubwa ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha dawa ambazo zitawahudumia watanzania pamoja na nchi za Afrika Mashariki na ya kati. Wawekezaji hao pia wanatarajia kuisaidia Tanzania katika uzalishaji wa chanjo ya ugonjwa wa homa ya Ini (Hepatics B na C ).
Kwa upande wake Waziri Ummy amewaahidi wawekezaji hao kuwasaidia katika mipango ya ujenzi huo na kutoa ushirikiano wa dhati katika kufanikisha viwanda hivyo vinajenga nchini kwa muda uliopangwa.
“Naelekeza kwa taasisi zote zitakazoguswa na uanzishwaji wa viwanda hivi watoe ushirikiano wa hali ya juu ili lengo hili lifikiwe,soko la dawa hapa nchini lipo naomba niwahakikishie hili”alisema waziri Ummy.
Waziri Ummy aliwaomba wawekezaji hao kuharakisha ujenzi wa viwanda huo na kujengwa ndani ya miezi kumi na nane kama walivyoahidi ili watanzania waanze kunufaika mapema.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika mazungumzo na Ujumbe huo wa wawekezaji toka nchini Misri kwenye ofisi ndogo ya wizara hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Wawakilishi toka wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) wakiwa katika mazungumzo hayo kwenye ofisi ndogo ya wizara ya afya, maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto iliyopo jijini Dar es Salaam
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika picha ya pamoja na Ujumbe huo wa wawekezaji toka nchini Misri na Wawakilishi toka wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) baada ya mazungumzo kwenye ofisi ndogo ya wizara hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam