Na Bashir Yakub
Ni kipindi muhimu kujua kuhusu hisa. Hivi karibuni utakuwa umesikia makampuni mbalimbali hasa yale ya simu yakiwatangazia watu kununua hisa. Ni muhimu kwako kujua kuhusu biashara hii. Huenda ikawa ya faida kwako au eneo zuri kwako kwa kuwekeza.
Mapema niseme kuwa usiogope wala usiwe mwenye hofu. Biashara ya hisa ni ya watu wote tajiri au maskini. Laki moja, laki mbili nk. unaweza kununua hisa. Ili umiliki hisa kwenye kampuni ya simu si lazima umiliki mamilioni kama unavyodhani. Na hapa ndipo tunapokosea na kuwaacha matajiri watambe nasi tubaki kulalamika.
1.HISA NI NINI.
Hisa ni mali kama zilivyo mali nyingine unazomiliki. Tofauti ya hisa na mali nyingine ulizonazo kama shamba, gari, nyumba nk.ni kuwa mali nyingine huweza kushikika au kuonekana kwa macho wakati hisa ni mali isiyoonekana kwa macho. Yumkini zote ni mali tu.
Hisa ni maslahi au haki fulani unayokuwa nayo katika taasisi au kampuni fulani. Ndiyo maana ni mali isiyoonekana kwasababu huwezi kuona maslahi au haki kwa macho.
2. KUMILIKI HISA KATIKA KAMPUNI.
Kampuni yoyote unayoiona huwa inao wanahisa. Wanahisa ndio wamiliki wa kampuni. Kwahiyo hata wewe ukinunua hisa kwenye kampuni yoyote na wewe unakuwa mmoja wa wamiliki.
Haijalishi ukubwa wa kampuni na kiwango chako cha hisa ulichonunua bali ni kuwa ukishanunua tu hapohapo na wewe unakuwa mmoja wa wamiliki. Hata hisa za laki moja nazo zinakufanya kuwa mmoja wa wamiliki.
Kiwango cha hisa zako ndicho kiwango cha umiliki wako. Kampuni ikiwa na hisa 100,000 na wewe ukamiliki hisa 50,000 basi wewe unaimiliki nusu ya kampuni. Ukimiliki hisa 25,000 basi wewe unamiliki robo ya kampuni. Halikadhalika ukimiliki hisa 500, 100, 50, 10, 5 au hata hisa 3 basi hichohicho kiwango chako cha hisa ulichonunua ndicho kiwango chako cha umiliki wa kampuni husika.
Kwahiyo ukinunua hisa 100 Vodacom basi wewe utaimiliki Vodacom kwa kiwango cha hisa hizo ulizonunua. Isipokuwa ni muhimu kujua kuwa anayemiliki hisa nyingi kuliko wote ndiye hujulikana kama mmiliki mkuu wa kampuni.
3. JE UTAFAIDIKAJE NA HISA.
Kila mwanahisa hupata gawio la faida pale kampuni inapotangaza faida. Kampuni hutangaza faida kila baada ya mwaka au nusu mwaka au vinginevyo.
Utapata mgao kwa asilimia kutokana na kiwango chako cha hisa ulizonazo. Ukiwa na hisa nyingi utapata mgao mkubwa, ukiwa na hisa kidogo utapata mgao mdogo na vivyo hivyo.
Kusoma zaidi BOFYA HAPA