Mkuu wa Wilaya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Taraba amepiga marufuku wananchi kuuza mazao ya chakula wanayovuna hususan mtama na badala yake waweke akiba.
Taraba alipiga marufuku hiyo jana wakati akifanya ziara katika kata za Lagana, Mwamashele, Mwakipoya na Masanga baada ya kubaini kuwepo kwa baadhi ya wananchi kufanya biashara hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Masanga alisema kuna baadhi ya watu huwahadaa na kununua mtama kwa bei ya juu hali inayowafanya wananchi wabaki bila chakula.
“Nasikia hapa kuna baadhi watu wanapita kwenu wananchi na kununua debe moja la mtama kwa shilingi elfu ishirini na tano msidanganyie na kuuza wewkeni akiba,” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Aidha alionya tabia ya baadhi ya watu kuuza mazao yakiwa shambani baada ya kukadiriwa kiasi cha mazao yao kabla ya kuyavuna aliwataka wananchi wakatae kufanya hivyo.
Kwa upande mwingine aliwataka kuandaa mashamba yao mapema na kupanda mazao yanayohimili ukame yakiwemo mtama ili yaweze kustawi na kuwapa chakula.
Taraba aliwataka wananchi hao kuwatumia wataalamu wa kilimo kwenye kata zao ili kupata ushauri wa kutumia mbegu zilizo bora ambazo zinaweza kuota na kukua kwa haraka.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (katikati) akizungumza na wananchi (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara kata ya Masanga. kulia ni Afisa Kilimo (Ubora wa mbegu), Maduhu Masunga
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (katikati) akizungumza na wananchi (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara kata ya Masanga. Wengine pichani kulia ni Afisa Kilimo (Ubora wa mbegu), Maduhu Masunga na Mwenyekiti wa kijiji cha Masanga, Gambishi Malele.
Mwananchi wa kata ya Masanga akitoa kero yake kwa Mkuu wa Wilaya, Nyabaganga Taraba wakati wa mkutano wa hadhara.