WAREMBO wanaotarajia kupanda jukwaani kesho Ijumaa kuwania taji la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" katika shindano litakalofanyika kwenye ukumbi wa Navy Beach kuanzia saa 2:00 usiku hapa jijini Dar es Salaam wanaingia kambini leo katika hoteli ya Hope Country iliyoko Kigamboni.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa mkuurugenzi wa hoteli hiyo ameamua kuwapatia malazi warembo wa kitongoji hicho ili kuwafanya waweze kujiandaa vyema na shindano hilo wakiwa pamoja na wametulia.
Alisema kwamba anaamini mshindi wa taji hilo mwaka huu atakiwakilisha vyema kitongoji hicho katika mashindano ya Redd's Miss Temeke na baadaye fainali za Taifa za Redd's Miss Tanzania zitakazofanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Somoe alisema kwamba Kamati ya Miss Kigamboni imejiandaa kufanya onyesho lililo na kiwango cha juu na wadau wa sanaa hiyo watarajie kuona mshindi anapatikana na kwenda kutetea taji la Redd's Miss Temeke kama iling'ara mwaka jana.
Aliitaja bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma itatumbuiza katika shindano hilo ambalo kiingilio cha viti maalum ni Sh. 10,000 na viti vya kawaida ni Sh. 5,000.
Mkurugenzi wa hoteli ya Hope Country, Geofrey Mugisha, alisema kuwa ameamua kudhamini shindano hilo kwa sababu yeye ni mkazi wa Kigamboni na anaamini kupitia shindano hilo washiriki watafanikiwa kutimiza ndoto zao.
Aliongeza kuwa mpaka sasa jumla ya warembo 12 wanaendelea na mazoezi hapa jijini chini ya Blessing Ngowi. Aliwataja washiriki watakaopanda jukwaani kuwania taji hilo ni pamoja na Rogathe Michael, Irene Rajab, Magdalena Olotu, Latifa Mohammed, Axsaritha Vedastus, Angella Lutataza, Sara Makembo, Amina Mussa, Ellen Sulle, Zuhura Masoud, Joyce Kamtonosye na Margareth Gerald.
Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu.
Baadhi ya wadhamini ambao wamethibitisha kusaidia shindano hilo ni pamoja na kampuni ya bia Tanzania kupitia kinywaji cha Redd's Premium Original, Montage Limited, Clouds Media Group, Papa Z , Silver Boutique, Jambo Leo, Machapta Production na Logikit.