MBUNGE wa Jimbo la Kigamboni, Faustine Ndungulile, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika onyesho la kumsaka malkia wa kitongoji cha Kigamboni mwaka huu "Redd's Miss Kigamboni 2013" katika shindano litakalofanyika Ijumaa Juni 7 kwenye ukumbi wa Navy Beach kuanzia saa 2:00 usiku hapa jijini Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na mbunge huyo amekubali kuja kubariki shindano hilo. Mratibu huyo alisema kwamba Kamati ya Miss Kigamboni imejiandaa kufanya onyesho lililo na kiwango cha juu na wadau wa sanaa hiyo watarajie kuona mshindi anapatikana na kwenda kutetea taji la Redd's Miss Temeke na baadaye kushinda taji la taifa. Alisema kuwa bendi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma itatumbuiza shindano hilo ambalo kiingilio cha viti maalum ni Sh. 10,000 na viti vya kawaida ni Sh. 5,000. Aliongeza kuwa mpaka sasa jumla ya warembo 12 wanaendelea na mazoezi hapa jijini chini ya Blessing Ngowi. "Shindano la Redd's Miss Kigamboni mwaka huu litakuwa bomba na wadau wasisite kujitokeza safari ya Miss Tanzania inaanzia katika kitongoji hichi Ijumaa hii," Somoe aliongeza. Aliwataja washiriki watakaopanda jukwaani kuwania taji hilo ni pamoja na Rogathe Michael, Irene Rajab, Magdalena Olotu, Latifa Mohammed, Axsaritha Vedastus, Angella Lutataza, Sara Makembo, Amina Mussa, Ellen Sulle na Zuhura Masoud. Warembo watano watakaoshika nafasi za juu kwenye shindano hilo watapata nafasi ya kushiriki kinyang'anyiro cha Redd's Miss Temeke baadaye mwaka huu. Wadhamini ambao wamethibitisha kusaidia shindano hilo ni pamoja na kampuni ya bia Tanzania kupitia kinywaji cha Redd's Premium Original, Montage Limited, Clouds Media Group, Papa Z , Silver Boutique, Jambo Leo, Machapta Production na Logikit. |
↧
Ndungulile mgeni rasmi Redd's Miss Kigamboni Ijumaa
↧