Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan M. Mwinyi akitia sahihi kwa niaba ya Serikali,Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Silaha ( ATT) Tanzania ilikuwa kati ya nchi 67 za kwanza ambazo zimetia sahihi katika siku ya kwanza ya uzinduzi wa tukio hilo la kihistoria. Baada ya Mkataba kutiwa sahihi nchi zaidi ya 50 kama sheria zinavyotaka utaanza kufanya kazi rasmi baada ya siku 90. Mkataba huu ambazo umechukua zaidi ya miaka sita hadi kupatikana unalenga katika pamoja na mambo mengine kusimamia na kuratibu biashara ya silaha zikiwamo mizinga ya kivita, magari ya deraya, ndege za kivita, helkopta za mashambulizi, meli za kivita na silaha ndogo na nyepesi. vile vile mkataba unalenga kudhibiti silaha zisiangukie mikononi mwa makundi ya kihalifu yakiwamo ya kigaidi
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa miongozi mwa nchi za kwanza kutia sahihi Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Silaha Duniani ( ATT)
Utiaji sahihi wa tukio hilo la kihistoria umeziduliwa jana jumatatu ( Juni 3) hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Ukishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Katika tukio hilo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwakilishwa na Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Utiaji sahihi wa mkataba huo unafanyika ikiwa ni takribani miezi miwili kupita tangu Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipoupitisha kwa kuupigia kura 154 za ndiyo na hivyo kuhitimisha majadiliano ya uundwaji wa mkataba yaliyodumu kwa takribani miaka sita.
Kutiwa sahihi kwa Mkataba huo sasa kunafungua fursa ya kuanza kufanya kazi rasmi baada ya siku 90, kwa sababu zilikuwa zikihitajika sahihi 50 ili upate baraka ya kuanza rasmi. Lakini idadi hiyo imepitiliza katika siku ya kwanza ya utiaji wa sahihi na kufikia nchi 67.
Dhumuni kuu la mkataba pamoja na mambo mengine ni kusimamia na kuratibu biashara ya silaha za aina mbalimbali zikiwamo, mizinga ya kivita, magari ya deraya, ndege za kivita, helkopta za mashambulizi, meli za kivita, makombora pamoja na silaha ndogo ndogo na nyepesi.
Aidha Mkataba pamoja masuala mengineyo hautaingilia uhuru wa nchi kununua silaha kwa matumizi yake ya ndani na haki ya kujilinda na kulinda mipaka yake, vilevile mkataba hauzui nchi kufanya biashara ya kusafiri aina yoyote ya silaha ilimradi inazingatia sheria na taratibu zilizomo ndani ya mkataba ikiwa ni pamoja na taratibu ambazo nchi yenyewe imejiwekea.
Matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa ni kwamba utekelezaji wa mkataba na kama utaekelezea ipasavyo utasaidia sana kudhibiti silaha zisiangukie mikononi mwa makundi mbalimbali ya kihalifu yakiwamo ya kigaidi.
Akizungumza mara baada ya kutia sahihi, Balozi Ramadhan Mwinyi aliungana na wasemaji wengine katika kukaribisha hatua hiyo muhimu. Huku akieleza kwamba kwa Tanzania kutia sahihi ni uthibitisho wa utayari wake wa kuutekeleza kwa kuzingatia masharti na matakwa yanayoendeana na mkataba huo.
Akasema Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kutia sahihi mkataba huo kwa kuwa ilikuwa moja kati ya nchi zilizodhamini Azimio la Kuanzishwa kwa Mkataba na pia ilishiriki kikamilifu katika majadiliano yote yaliyozaa mkataba huo.
Balozi Mwinyi akaeleza pia kuwa kufanya kazi kwa Mkataba huo kutachangia katika amani ya Kimataifa, amani na usalama wa Kikanda na pia utachangia sana katika kupunguza madhara yatokanayo na biashara haramu na holela ya silaha lakini pia utasaidia katika kukuza na kuimarisha uhusiano mzuri miongoni mwa nchi wanachama.
Katika hatua nyingine Muwakilishi huyo wa Tanzania amesisitiza haja na umuhimu wa uwepo wa fursa sawa kati ya wasafirishaji wa silaha na waagizaji wa silaha na kwamba Mkataba huo usidhibiti au kuzuia biashara ya silaha ambayo ni halali na kwamba mkataba haupashwi kuingilia au kwa namna yoyote ile au kuadhiri uhuru na haki ya nchi kujilinda na kulinda watu wake.
Tanzania pia imekaribisha misaada ya kiufundi katika maandalizi ya utekelezaji wa mkataba huo hasa kwa nchi zinazoendelea.
Nchi hizo 67 ambazo zimetia sahihi ni , Albania, Antigua and Barbuda, Argentina, Australia, Austria, Bahamas, Belgium, Belize, Benin, Brazil, Burkina Faso, Burundi, Chile, Costa Rica, Cote D’ Ivoire, Croatia, Cyprus, Czech Republic , Denmark, Djibout, na Dominica Republic.
Nyingine ni Estonia, Finland, France, Germany, Greece, Grenada, Guyana, Hungary, Iceland, Italy, Jamaica, Japan, Latvia, Liechtenstein, Lithuania, Luxembourg, Mali, Malta, Mauritania, Mexico na Montenegro.
Mataifa mengine ni Mozambique, Netherlands, New Zealand, Norway, Palau, Panama, Portugal, Republic of Korea, Romania, Saint Lucia, Saint Vincent and the Grenadines, Senegal, Seychelles, Slovenia, Spain, Suriname, Sweden, Switzerland, Togo, Trinidad and Tobago, Tuvalu, United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland, United Republic of Tanzania na Uruguay
.