Jamhuri ya Singapore (mji mkuu wake pia ni Singapore) ni nchi ya kisiwan Kusini Mashariki ya bara la Asia, ikiwa kusini mwa ncha ya Peninsula ya Malai na kilometer 137 kutoka mstari wa Equator. Ukubwa wa kisiwa kikuu cha Singapore ni km42 kwa urefu, wakati upana ni km23, na kina ukubwa wa kilomita za mraba 586.5. Ukubwa wake kwa jumla ukichanganya na visiwa vyake vyote ni kilomita za mrada 646.1(Zanzibar ina ukubwa wa kilomita za mraba 1464, ikiwa ni urefu wa km 86 na upana wa km36).
Singapore ni nchi inayofanywa na visiwa 63, ikiwa imetenganishwa na nchi ya Malaysia na ghuba ya Johor kwa upande wa kaskazini na visiwa vya Riau vya Indonesia katika ghuba ya Singapore upande wa kusini. Ni nchi ya vikwangua anga ambayo imeanza mambo ya biashara miaka ya 1819, ambapo mwaka 1824 Waingereza waliitawala. Baada ya kukaliwa na Japan katika vita vya pili vya dunia nchi hii ndogo ilijipatia uhuru wake mwaka 1963, ambapo miaka miwili baadaye ikaja kujitenga na Malaysia waliyokuwa wakitawaliwa nayo kwa pamoja na Uingereza.
Toka wakati huo imeendelea na kuwa moja ya nchi tajiri duniani, na ni mojawapo ya nchi nne zijulikanazo kama Chui wa Asia. Singapore ni nchi ya nne duniani kama kituo kikuu cha biashara, ambapo bandari yake ni moja kati ya tano ambazo zinafanya kazi sana duniani. Uchumi wake zaidi unategemea biashara ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi na bandari.
Hivi sasa Singapore ni ya tatu duniani kwa kuwa na watu wenye kipato kikubwa. Sifa zingine za nchi hii ni kuwa ya pili duniani kwa wingi wa ma Casino na kumbi za kuchezea kamari, ni mojawapo ya vituo vitatu vikubwa vya kuchujia mafuta na pia wanaongoza katika kufanya mategenezo ya meli. Benki ya dunia tayari imeitaja Singapore kama nchi iliyo nyepesi kufanya ama kufanyia biashara, na inaongoza kwa mambo ya biashara ya fedha za kigeni, ikiwa nyuma ya London, New York na Tokyo.
Asilimia kubwa ya wakaazi wake ni Wachina, wkifuatiwa na watu wa mataifa ya Asia kama Wahindi, Malay na wengineo. Katika sense ya mwaka 2011, idadi ya watu wa Singapore ilikuwa milioni 5.18, ambapo milioni 3.25 ama asilimia 63 ni raia, na waliosalia (37%) ni wakaazi wa kudumu ama wafanyakazi wa mataifa mengine. Asilimia 23 ya raia wa Singapore walizaliwa nje ya nchi hiyo. Na hiyo huchanganyi na watu milioni 11 wanaotembelea kisiwa hicho kila mwaka. Lugha rasmi za Singapore ni nne. Kichina (49.9%) Kiingereza(32.3%) Ki-Malay (12.2%) na Tamil.
Kwa kuwa Singapore ni Kisiwa kidogo kinachokaliwa na watu wengi, idadi ya magari binfasi iko chini sana kwani uthibiti wake si mchezo ili kupambana na uchafuzi wa hali ya hewa na foleni. Yaani mtu akitaka kununia gari binfasi inabidi alipe ushuru ambao ni mara moja na nusu ya bei ya hilo gari. Pia inabidi apate hati ya kukaa nalo hilo gari ya miaka 10, na bei ya kununulia hiyo hati ni sawa na bei ya gari aina ya Porsche huko Marekani! Yaani bei ya gari binfasi Singapore ni ya juu kuliko nchi yoyote inayoongea Kiingereza duniani. Hivyo ni mtu mmoja tu katika 10 mwenye gari binafsi.
Cha kufurahisha ni kwamba kuna sheria kadhaa zinazodumisha nidhamu na usafi wa mazingira nchini Singapore. Ya kwanza ni kosa la jinai kutumia choo na kukiacha bila ku-flush. Ukikamatwa unapigwa faini hadi upate kizunguzungu. Ni kazi ya Askari polisi kuhakikisha vyoo vya umma viko safi kila mara.
Sheria ingine kali ambayo ilitungwa toka mwaka 1968 ili kuhakikisha nchi inabaki safi ni hii ya usafi. Ni kosa la jinai kutupa taka ovyo barabarani. Faini yake ni dola 1,000 na pia unaweza ukaadhibiwa kutumikia adhabu ya kufanya kazi za kijamii. Ukitenda kosa hilo mara tatu unavalishwa alama inayosema “Mimi ni mchafuzi wa mazingira”
Kula pipi ubani (Big G ama bazooka) nako kuna sheria zake, kwanza zimepigwa marufuku kuuzwa hovyo hovyo. Ukitaka unakwenda duka la madawa na unapoitafuna hakikisha masalia unayatupa kwenye pipa la taka. Ukikutwa umetema barabarani unapigwa bonge la faini.
Mambo ya kukumbatiana na mpenzi wako hadharani pia ni marufuku. Hayo mambo kafanyieni ndani kwenu. Ukikutwa ni faini na hata kifungo jela. Haya ni baadhi tu ya maajabu ya Singapore ambako Ankal anakula vekesheni yake huku akiwa makini asibambwe kafanya kosa la aina hizo hapo juu.
Sehemu ya jiji la Singapore linavyoonekana usiku
Ankal akiwa katikati ya jiji la Singapore usiku wa kuamkia leo |
Ni saa moja na nusu asubuhi ya leo Jumanne (Bongo ni saa 10 za Alfajiri) na Ankal analishangaa jiji la Singapore kabla ya kuweka ze fulanazzz pembeni na kuanza kula tizi la nguvu.