Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 115279

Serikali yaahidi kusaidia zaidi makandarasi nchini

$
0
0
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam Serikali imesema itaendelea kuhakikisha makandarasi wazalendo wanaendelea kupata msaada unaotakiwa ili kuendeleza sekta ya ujenzi hapa nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Pombe Magufuli alipokua akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa majadiliano wa bodi ya makandarasi Tanzania uliomalizika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Serikali inathamini kazi yenu na itaendelea kuwaunga mkono kila inapowezekana,” alisema.

Dkt. Magufuli alisema serikali imetenga kiasi cha Tshs 500.4 bilioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya mfuko wa barabara kwa mwaka huu na kuahidi kuwa miradi hiyo itafanywa na makandarasi wa ndani.

Alisema kila serikali duniani inasaidia watu wake na serikali ya Tanzania itafanya kila juhudi kusaidia makandarasi wa ndani kama njia ya kusaidia wananchi wake.

“Mkipewa kazi hakikisheni mnafanya vizuri na kwa kufuata maadili, kanuni na sheria,” alisema.

Alisema haiwezekani asilimia 60 ya kazi katika sekta ya ujenzi kumilikiwa na makandarasi wa nje wakati wao ni asilimia 10 tu ya makandarasi hapa nchini. Kuna jumla ya makandarasi wazalendo 7,000 hadi sasa.

Hata hivyo aliihimiza bodi ya makandarasi kuendelea kufuta usajili wa kampuni za makandarasi ambazo zinakiuka maadili ya kazi ili kulinda uchumi wa nchi na kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

“Endeleeni na kufuta usajili wa wale wanaokiuka maadili...nawapongeza kwa hili,” alisema.

Alizitaka benki hapa nchini kuonyesha uzalendo kwa kubuni njia za kuwasaidia makandarasi na pia kulegeza masharti ya mikopo kwao. Kwa upande wake, Msajili wa CRB, Injinia Boniface Muhegi alisema ni vyema makandarasi waheshimu ushauri wa kitaalamu wanaopewa ili kuweza kutekeleza kazi zao kwa ufanisi.

Alisema kuanzia sasa bodi yake itakaza uzi kwenye usajili wa makandarasi na kuwafanyia tathmini kila baada ya miaka mitatu. Pia alisema kuanzia sasa bodi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika zitahakikisha kuwa hakuna mkandarasi mmoja atakaerundikiwa kazi nyingi wakati wengine hawana na kusema kuwa rushwa itapigwa marufuku kwa nguvu zote.

Awali, Mwenyekiti wa bodi ya CRB, Eng. Consolata Ngimbwa alissitiza makandarasi nchini kuungana ili kuwa na nguvu na pia kuweza kushindana na wale wa nje ambao wengi wao wana nguvu za mitaji, na utaalamu.

“Tuungane ili na sisi tuweze kupata sifa za kupata miradi mikubwa,” alisema.

Akifafanua zaidi alisema kuwa makandarasi wa madaraja ya juu washirikishe wale wa madaraja ya chini ili waweze kufanya kazi pamoja kwa faida yao wote na kwa faida ya taifa kwa ujumla.

“Makandarasi wa madaraja ya juu waruhusu ushirika na wale wa madaraja ya chini ili kuleta mafanikio zaidi,” alisema. Mkutano huo wa siku mbili ulilenga kuangalia changamoto na mafanikio katika sekta ya ujenzi Tanzania ndani ya miaka kumi na tano iliyopita.

Mapendekezo ya mkutano huo yatapelekwa kwa wadau husika na baadae kufuatilia utekelezaji wake. Takwimu zinaonyesha kwamba sekta ya ujenzi inachangia asilimia saba ya pato la taifa huku ukuaji wake kwa mwaka ikikadiliwa kuwa ni asilimia kumi na moja ikiwa ni sekta ya pili kwa kasi ya ukuaji huku sekta ya madini ikiongoza. Asilimia sitini ya bajeti ya maendeleo nchini inakwenda kwenye sekta ya ujenzi huku asilimia themanini ya fedha hizo zikienda kwa wanachama wa bodi ya usajili wa mandarasi wa ujenzi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 115279

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>