MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la Mastaa chipukizi zaidi ya 320 litafanyika Jumapili 26, 2013 katika ukumbi wa Starlight Hotel kuanzia saa 4 asubuhi.
Mwenyekiti wa Shiwata, Caasim Taalib alisema Madabida ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) atapata nafasi ya kuona vikundi mbalimbali vya sanaa kikiwepo kikundi cha Kaole, Splendid, Super Shine Taarab pamoja na wasanii mbalimbali wa Bongo Flava, Maigizo,Ngoma, Dansi na Sarakasi nao wamethibitisha kushiriki.
Taalib alisema wasanii wakongwe wa bongo flava walioalikwa ni Stara Thomas, Safi Theatre Group, Ommy G na waigizaji wakongwe wa Kaole na Splendid wataonesha umahiri wao katika fani ya sanaa Kauli Mbiu ikiwa ni Kilio cha Msanii .
Vikundi vingine vitakavyonesha vipaji vyao ni Kepteni Shaibu, Tanzania Disabled, Uyoga Boga Village, Ndafu Arts Group, CGC, Magengistar Crew, Dodo Arts Group, Culture Arts Group, Wachapa Kazi Academy, Soweto Picture, Shiwata Commedy, Mwavionelachi, Manuari Arts Group, Tandale Morden Taarab na Begeja Wushu, Taalib alisema tamasha hilo ambalo limepata kibali cha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pia wamealikwa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania,Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),Shirikisho la Muziki Tanzania na Shirikisho la Sanaa za maonesho Tanzania.
Mwenyekiti aliwaomba viongozi wengine wa bendi za muziki, taarab, vikundi vya sanaa,mapromota,maprodusa na wadau wote kushiriki katika tamasha hilo ili kujenga ushirikiano wa pamoja.