Na Abdulaziz Video,Ruangwa
Jumla ya wanafunzi 212 Kati ya 449 wanaosoma kati ya darasa la tatu hadi la saba katika Shule za Msingi za Nandagala na Mkata Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi hawajui kusoma wala kuandika huku wengine 15 ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.
Hayo yamebainika katika kikao cha wadau wa Elimu Wilayani Ruangwa kilichokaa chini ya Mwenyekiti wake,Mkuu wa Wilaya hiyo Agness Hokororo Kupokea taarifa za hali ya Elimu na kutafuta Ufumbuzi wa chaongamoto zinakwamisha Elimu Wilayani humo kilichofanyika jana.
Wakichangia katika kikao hicho Baadhi ya Wadau wakiwemo Madiwani wa Halmshauri hiyo walieleza kuwa Mwamko Mdogo wa Wazazi na Uwezo mdogo wa Walimu katika Ufundishaji ikichangiwa na Upungufu mkubwa wa walimu pamoja na Mila na Desturi ni baadhi ya changamoto zinazokwamisha ukuaji wa Elimu Wilayani Humo.
Andrew Chikongwe,Diwani Kata ya Nandagala alisema kuwa tatizo lipo kwa walimu kwani wengi wao hawajitumi katika ufundishaji licha ya kuwepo kazini muda wote hali inayoonyesha kuwa wana mgomo baridi. “Pamoja walimu kuwepo kazini lipo tatizo la kutojituma katika ufundishaji hii inachangia sana watoto wetu wafanye vibaya”alisema Chikongweali.
Naye Juma Nampupanga ambaye ni Mfanyabiasharaalisema kuwa kutotilia mkazo wa elimu miongoni mwa wananchi ni kikwazo kikubwa kwa mafanikio ya watoto wetu kwani wananchi wengi wa wilaya ya Ruangwa hawana mwamko wa elimu kwani si kipaumbele cha hivyo kutofuatilia maendeleo ya watoto.
Ibrahimu Ndoro Diwani wa Kata ya Ruangwa aliitaka serikali kuwachulia hatua baadhi ya walimu wanaopangwa kufanya kazi katika Wilaya za mikoa ya kusini ambao mara wakisharipoti huwa wanaondolka kwa kisingizio cha kufuata familia zao na badala yake hawarudi tena na kufanya wilaya hizo kuendelea kuwa na upungufu wa waalimu.
Akizungumza kwenye mkutano huo mkuu wa wilaya hiyo Agnes Hokororo aliwataka wananchi na viongozi kushirikiana katika kuondoa changamoto mbalimbali zinzosababisha maendeleo mabaya ya elimu wilayani humo.
“Iwapo viongozi tutashirikiana maendeleo ya elimu wilwywni kwetu yatakuwa mazuri kwani suala la maendeleo ya elimu ni la kila mmoja wetu”alisema Hokororo
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa,Agness Hokororo(MB) Akiendesha kikao cha wadau wa Elimu wilayani Ruangwa Mkoani Lindi.
Baadhi ya Wadau wa Elimu wilayani Ruangwa Mkoani Lindi,wakifatilia kikao hicho.