Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman, akisalimiana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi na baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania mkoani humo walikokuja kumpokea jana Katika Ofisi ya Ikulu ndogo ya Mkoa wa Katavi kuanza ziara yake ya kikazi ya kutembelea Mahakama na kujionea hali ya utoaji haki mkoani humo, mbele ya Mhe. Jaji Mkuu ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Paza Mwamlima ( picha na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania).
Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Majaji na Mahakimu nchini kusikiliza kesi na kuzitolea maamuzi kwa wakati ili kuondokana na mlundikano wa mashauri ambao pia unasababisha pia mlundikano wa Mahabusu gerezani.
Wito huo umetolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, akiwa Katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua Mahakama katika Mikoa ya Mbeya, Rukwa na Katavi hivi karibuni.
"Mahakama imejipanga Katika kuhakikisha kuwa kila kesi inayoingia Mahakamani isizidi zaidi ya miaka miwili, hii ni Katika kuhakikisha kuwa tunaondokana na mlundikano wa mashauri katika Mahakama zetu nchini," alibainisha.
Aliongeza kuwa, hivi karibuni Maafisa mbalimbali wa Mahakama walitembelea Mahakama nchi nzima ili kupata takwimu za kesi za muda mrefu, lengo ni kuwa kumaliza mashauri yote ya nyuma ndani ya miaka miwili ijayo.
Hata hivyo, Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa suala la kumaliza mashauri kwa wakati ni jambo ambalo linahitaji ushirikiano wa karibu baina ya wadau wote wa sheria kuanzia Ofisi ya upelelezi, DPP na kadhalika.
Aliainisha juu ya maeneo muhimu ambayo yanaweza kutatua tatizo la mlundikano wa mashauri ikiwa ni pamoja na kuboresha Masjala za Mahakama jambo ambalo linaenda samba samba na utunzaji bora wa Mafaili ya kesi, kuboresha maslahi ya Majaji na Mahakimu pamoja na Watumishi wote wa Mahakama kwa ujumla.
Pamoja na hayo, Mhe. Jaji Mkuu aliainisha madhumuni ya ziara yake kuwa ni kutathmini kazi ya utoaji haki kwa ngazi zote za Mahakama, kuongea na Watumishi ili kuainisha changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.
Miongoni mwa changamoto zilizoibuliwa Katika ziara hiyo ni pamoja na uchakavu wa majengo ya Mahakama, maslahi duni kwa watumishi wa Mahakama na mengineyo.
Katika ziara yake Katika Mikoa hiyo Mhe. Jaji Mkuu aliambatana na Naibu Mkurugenzi wa Mahakama za Wilaya hadi Rufaa, Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo, Afisa Tawala ili kujionea maeneo hayo na hatimaye kuhaidi kufanyia kazi changamoto zilizoainishwa.