Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye akizungumza na wasomi wa chuo cha Tumaini hivi sasa
Na Francis Godwin
Waziri Mkuu mstaafu, Mhe Frederick Sumaye amewafunda wasomi wa chuo kikuu Iringa zamani Tumaini kuwa watumie kanisa hilo litakalojengwa kwa ajili ya kueneza amani zaidi huku akiwataka kuachana na malalamiko yasiyokwisha yanayotokana na baadhi yao kutojituma katika kazi.
Mhe Sumaye ametoa kauli hiyo leo katika hotuba yake kwa wasomi wa chuo kikuu cha Iringa cha Tumaini kabla ya kuanza kuendesha harambee kwa ajili ya ujenzi wa kanisa la chuo hicho.
Amesema kuwa katika Bibilia rushwa na ufisadi ni dhambi kubwa katika Taifa na kuwa vitu hivyo tunavilea wenyewe japo kuna tatizo kubwa na kuwa kaburi pekee la mambo machafu ni ujenzi wa kanisa hilo na matumizi yake kutumika kwa malengo ya kuhubiri amani na kukemea ufisadi.
" Mfano ni nani kati yenu amepata kutozwa rushwa na mkulima ila rushwa inatozwa na wenye nafasi na hivyo lazima vijana wasomi mkumaliza hapa lazima kwenda kubadilisha Taifa....ndio maana nilipoitwa na baba askofu kwa ajili ya changizo la kanisa nikasema nitafika kwani ni jambo jema" Mhe.
Sumaye alisema na kuongezea kuwa kumshangilia mtu anayeendesha gari la kifahari alilolipata kwa njia ya wizi ni hatari na kuendelea kuliangamiza Kanisa.
Alisema kuwa hivi leo watu wanajenga chuki kati ya wanyonge na matajiri na kuwa limezuka jambo baya zaidi kwa watu kuchukiana kwa misingi ya dini zao na kuwa nchi yeyote itakayoingia katika machafuko ya imani ni hatari zaidi.
Mhe Sumaye alisema kuwa vita ya kiimani ni mbaya zaidi na siku zote vita hiyo huwa haina mshindi hivyo ni vema kila dini kuanza utaratibu wa kuwafundisha vijana wake ili kuwa na uzalendo katika Taifa hili.
Aidha alisema kuwa malumbano ya kidini yanayoendelea mbali ya kutokuwa na mshindi ila bado vita hiyo haitakuwa na mshindi na hivyo ni vyema kila mmoja kuachwa akiendelea kuamini kile ambacho ana amini hata kama ni chini ya mti asisumbuliwe.
Alisema vita ya udini inayoendelea kwa sasa ni mbaya zaidi na kuwa watanzania tusiruhusu vita hiyo kupandikizwa .
Mbunge wa jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa akiwa katika harambee ya ujenzi wa kanisa chuo cha Tumaini ambako mgeni rasimi ni waziri mkuu mstaafu Mhe Frederick Sumaye
Mbunge Msigwa akisalimia katika harambee hiyo
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa Dkt Mdegella ,waziri mkuu mstaafu Mhe Frederick Sumaye na mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Ishengoma wakiwa katika harambee hiyo. Picha na Francis Godwin.